AMERICARES YATOA MATIBABU BILA MALIPO KWA WAGONJWA WA FISTULA MKOANI SHINYANGA

Na Mwandishi wetu – Malunde 1 blog

Shirika
la Americares limeendesha zoezi la utoaji
 wa huduma ya matibabu ya bila malipo
na kufanya operesheni ya ugonjwa
 wa fistula kwa kina mama waliobainika kuwa na
ugonjwa huo ndani ya mkoa wa Shinyanga.

Zoezi
hilo la matibabu limefanyika kwa muda wa siku
 tatu katika hospitali ya Rufaa
ya Mkoa wa Shinyanga iliyopo kata ya Mwawaza manispaa ya Shinyanga.

Mratibu
wa zoezi hilo la matibabu bi. Halima Khamis ambaye pia ni Mratibu wa Afya ya Uzazi ya Mama na Mtoto Mkoa wa Shinyanga amesema kufuatia uwepo wa malalamiko na
changamoto ya ugonjwa wa fistula kwa baadhi ya akina mama mkoani humo ndipo
walichukuwa hatua na kuamua kusogeza huduma hiyo.

“Kutokana
na uwepo wa malalamiko na changamoto ndipo tukachukua hatua kama Wizara ya Afya pamoja na ofisi ya mkuu wa mkoa kwa kushirikiana na wadau wetu Americares
na hospitali ya kanda Bugando tukaona tuweke kambi hii ili kuwafikia Akina mama
wenye ugonjwa wa fistula ambapo mpaka sasa tumefanikiwa kupata akina mama
24 waliojitokeza kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya upasuaji wa ugonjwa huu.

“Pamoja
na kutoa elimu ya afya tuliweza kutoa matangazo kupitia vyombo vya habari ambapo
mpaka sasa tumepata Akina mama 24 waliojitokeza kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya
upasuaji wa ugonjwa wa fistula”,
ameongeza Halima Khamis.

Mwakilishi kutoka
Shirika hilo la Americares Dkt. Jonas Kagwisage, amesema wana miaka 13 sasa
wamekuwa wakitoa huduma hiyo ya Matibabu bure ya Fistula kwa wanawake kwa
kushirikiana na Madaktari Bingwa wa wanawake kutoka Hospitali ya Rufaa ya
Bugando, na sasa wamefanya kambi mkoani Shinyanga kutoa huduma hiyo.

Amesema katika Mkoa
wa Shinyanga wameanza Kambi hiyo tangu Juni 23 na itahitimishwa kesho Juni 29,2024 na kwamba hadi sasa wameshawafanyia Upasuaji wa Ugonjwa huo wa Fistula wanawake
16 na leo watawafanyia wengine nane na kufikisha idadi ya wanawake 24.

Daktari Bingwa wa
Magonjwa ya Wanawake kutoka Hospitali ya Rufaa Bugando Jijini Mwanza Dk. Elieza
Chibwe, amesema tatizo la Ugonjwa wa Fistula bado ni kubwa sana kwa wanawake na
husabishwa na uchungu pingamizi kwa mwanamke anapokuwa mjamzito, na hutokea
Tundu ambalo linaunganisha njia ya uzazi na sehemu ya haja kubwa na ndogo na
Mwanamke hutokwa na haja kubwa na ndogo muda wote.

 

“Ugonjwa huu
husababishwa na uzazi pingamizi wakati wa kujifungua au kutopata huduma kutoka
kwa mtaalam wakati wa kujifungua kwa maana ya kujifungulia nyumbani au
kujifungua bila msaada wa mtaalam na kupelekea kupasuka kwa njia ya uzazi na
kusababisha kutoka haja ndogo mfululizo, ugonjwa wa Fistula ni ugonjwa wa Aibu
na Matibabu ya Fistula ni Upasuaji tu, na tunataka hadi kufikia 2030 tatizo la
Fistula liwelimekwisha kabisa,
”amesema Dkt. Chibwe.

Naibu Meya wa Manispaa
ya Shinyanga Zamda Shabani, amelishukuru Shirika la Americares kwa kufadhili wa
Tiba hiyo, pamoja na Madaktari kutoka Bugando na kutoa wito kwa wanawake
wajitokeze kwa wingi kupata huduma hiyo,ili waondokane na tatizo hilo na
kufanya shughuli zao kwa uhuru huku Diwani wa Mwawaza Juma Nkwabi, ameiomba
Serikali ipeleke pia Madaktari Bingwa wa kutoa huduma ya Fistula katika
Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, na kutotegemea Madaktari wa
Bugando.

Naye Mmoja wa wanawake ambaye amefanyiwa upasuaji Terezia
Mayunga kutoka wilayani Kahama, amesema ameishi na tatizo la Fistula kwa miaka
38, lakini sasa amepatiwa Tiba na hali yake ni nzuri, huku mwingine akibainisha
kwamba baada ya kupatwa na tatizo hilo mumewake alimkimbia na sasa amepona na
kushukuru Shirika la Americares na Madaktari kwa kumpatia tiba bure.


Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake kutoka Hospitali ya Rufaa Bugando Jijini Mwanza Dk. Elieza Chibwe akizungumza.

Mwakilishi kutoka Shirika hilo la Americares Dk. Jonas Kagwisage akizungumza.

Mganga mfawidhi hospitali ya Rufaa mkoa wa Shinyanga Dkt. Luzila John akizungumza hospitalini hapo.


Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Faustine Mlyutu akizungumza wakati wa zoaezi hilo.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Faustine Mlyutu akizungumza wakati wa zoaezi hilo.

Naibu Mstahiki Meya Manispaa ya Shinyanga Zamda Shabani akizungumza wakati wa zoezi hilo.

Diwani kata ya Mwawaza Juma Nkwabi akizungumza wakati wa zoezi hilo.



Baadhi ya waliopatiwa matibabu





Picha ya pamoja.

Related Posts