WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kwa mwaka 2023/2024 hadi kufikia Juni, 2024 jumla ya wanafunzi 224,056 wamepatiwa mikopo yenye jumla ya Sh 743.2 bilioni sawa na asilimia 94.6 ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Mikopo hiyo ni kwa ngazi ya stashahada, shahada ya awali, stashahada ya juu ya mafunzo ya Sheria kwa vitendo, shahada za umahiri na uzamivu, na ufadhili wa Samia (Samia Scholarships) katika masomo ya sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati.
Majaliwa amebainishwa hayo leo Ijumaa wakati akitoa hotuba ya kuahirisha mkutano wa 15 wa Bunge jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi tarehe 27 Agosti mwaka huu.
Amesema kwa mwaka 2024/2025 Bunge limepitisha kiasi cha Sh 787 bilioni kwa ajili ya kukopesha wanafunzi 250,000 ikijumuisha wanafunzi wapya wa shahada ya kwanza wapatao 80,000.
Amesema maandalizi ya awali yameanza ikiwa ni pamoja na: kusambaza mwongozo wa upangaji na utoaji mikopo; kufungua dirisha la uombaji mikopo kwa mwaka 2024/2025 kwa muda wa siku 90 kuanzia tarehe 1 Juni hadi 31 Agosti, 2024; kutoa elimu kwa waombaji mkopo na wadau wengine.
Kwa upande wa urejeshaji mikopo, amesema Bodi ya Mikopo imeendelea kukusanya mikopo iliyoiva kutoka kwa wanufaika wa mikopo.
“Kwa mwaka 2023/2024 Serikali ilipanga kukusanya kiasi cha Sh 230 bilioni ambapo hadi kufikia Mei 2024 jumla ya Sh 161 bilioni zilikusanywa sawa na asilimia 70 ya lengo.
“Ili kuimarisha ukusanyaji wa mikopo, Serikali imeweka mikakati kadhaa ikiwemo kuwakumbusha waajiri kuwasilisha majina ya wanufaika ndani siku 28 baada ya kuwaajiri; kushirikiana na kuunganisha mifumo na wadau wa kimkakati kama vile NIDA, TRA, taasisi binafsi za ndani na nje ya nchi; kufanya kampeni za kuwafichua wanufaika; kutoa elimu kupitia mitandao ya kijamii; na kufanya kaguzi kila mwezi kwa waajiri wa sekta ya umma na binafsi,’ amesema.