Dar/Katavi. Familia ya Edgar Mwakabela, maarufu Sativa anayedaiwa kutoweka Juni 23 na kupatikana mkoani Katavi, imesema inasubiri ripoti ya madaktari kujua lini ataletwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
Mwakabela, mkazi wa Mbezi wilayani Ubungo ni maarufu katika mtandao wa X (zamani twitter) kwa jina la Sativa alipatikana Alhamisi Juni 27, 2024 akiwa na majeraha mwilini, akiomba msaada wa kupelekwa hospitali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani alisema jana taarifa zaidi zitatolewa baada ya kupata ripoti ya daktari.
“Tulipata taarifa kutoka kwa watu kuwa wamekuta mtu mwenye majeraha hajiwezi yupo katika Hifadhi ya Katavi. Askari walifika eneo la tukio kumhoji. Amesema alichukuliwa na watu wakaenda Arusha kutoka hapo walimpiga akapoteza fahamu alivyozinduka akajikuta yupo msituni akahangaika kujivuta hadi barabara alipokutana na wananchi,” alisema Kamanda Ngonyani.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Juni 28, 2024 Patrick Israel, kaka mkubwa wa Sativa amesema ndugu yake anaendelea vema na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi.
“Anaendelea vema na yupo katika uangalizi mzuri wa madaktari wanaohakikisha afya yake inarejea katika hali ya kawaida. Leo jioni huenda tukapata ripoti kuhusu mwenendo wa hali yake kutoka kwa madaktari kisha tutajua lini ataletwa Dar es Salaam kwa huduma za kitabibu zaidi,” ame.
“Akiendelea vizuri tutawaambia Watanzania lini ataletwa Dar es Salaam, lakini tunawasihi wananchi kuendelea na maombi kwa ndugu yetu ili apone na kurudi katika majukumu yake,” amesema Israel.
Dk Parason Willison wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi anakotibiwa Sativa, amesema anaendelea vema.
“Kupitia vipimo alivyofanyiwa amegundulika amevunjika taya na mguu, pamoja na kuwa na majeraha katika mwili wake, lakini hali yake inaendelea vema baada ya kumpa matibabu na yupo katika uangalizi maalumu wa madaktari,” amesema.
Dk Willison amesema hali ya Sativa inazidi kuimarika tofauti na alivyopelekwa hospitali hapo akitoke Kituo cha Afya cha Mpimbwe.
Amesema hivi sasa anaweza kujihudumia baadhi ya mahitaji yake.
“Kikubwa tuwaombe ndugu, jamaa na marafiki wasiwe na wasiwasi, wawe wavumilivu wakati Mwakabela akiendelea kupatiwa matibabu ili kurejea katika hali yake ya kawaida,” amesema Dk Willison.
Katika hatua nyingine, Israel amesema hadi leo saa saba mchana wamekusanya zaidi ya Sh10 milioni kutoka kwa wananchi kwa ajili ya matibabu ya Sativa kupitia harambee iliyoanza jana Alhamisi saa saba mchana.
“Kumekuwa na mwitikio mzuri, nawaomba ndugu, jamaa na marafiki waendelea kujitoa na kutuunga mkono katika mchango kufanikisha matibabu ya Sativa atakapofika Dar es Salaam,” amesema Israel.
Akizungumza baada ya kupatiwa matibabu Sativa amesema alitekwa Juni 23 saa moja usiku alipokuwa akielekea nyumbani kwake, akidai kuchukuliwa na watu wasiojulikana.
Amedai watu hao walimshikilia kabla ya kumpiga risasi na kumuacha alfajiri ya kuamkia Alhamisi, Juni 27 katika Hifadhi ya Katavi.
“Namshukuru Mungu na Watanzania wote, tangu Jumapili sikuwa hewa lakini wamenipambania Mungu awabariki haya yote ni kutokana na kazi yangu ninayoifanya kwenye mitandao ya kijamii.”
“Mimi siyo mwanaharakati ila napenda vitu wanavyofanya harakati, naunga mkono vitu wanavyofanya. Inawezekana ikawa ndiyo chanzo cha kutekwa ila sina ugomvi na mtu yeyote, Mungu bado ananipenda ndiyo maana bado nipo hai hadi sasa,” amesema Sativa.
Suala la kutoweka na kupatikana kwa Sativa limezua mjadala kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya wananchi wakihoji kama masuala ya utekaji bado yapo nchini.
Baadhi yao wamelifananisha tukio la Sativa na la Desemba 26, 2021 la kupotea waliokuwa mafundi simu na wafanyabiashara eneo la Kariakoo, Dar es Salaam waliodaiwa kutekwa na watu waliokuwa wamevaa sare za polisi.
Vijana hao ni Tawfiq Mohamed, Self Swala, Edwin Kunambi, Hemed Abass na Rajabu Mdoe na siku ya mwisho mmoja wao alituma ujumbe kupitia simu ukieleza wamekamatwa maeneo hayo wakiwa kwenye gari IST nyeusi na wanapelekwa Kituo Kikuu cha Polisi.