Guede kumpisha Sowah Yanga | Mwanaspoti

YANGA ipo kwenye mazungumzo ya kumpata mshambuliaji raia wa Ghana, Jonathan Sowah kwa mkopo wa mwaka mmoja kutoka Al-Nasr Benghazi ya Libya aliyojiunga nayo Januari mwaka huu kwa mkataba wa miaka miwili akitoka Medeama.

Inaelezwa endapo dili lake litakamilika, kuna uwezekano mkubwa wa Yanga kutemana na raia wa Ivory Coast, Joseph Guede aliyejiunga na Yanga Januari mwaka huu akitokea Tuzlaspor FC ya Uturuki na kufunga mabao sita ya Ligi Kuu Bara. Lakini hata Kennedy Musonda na yeye huenda akapigwa chini muda wowote wiki ijayo.

Sowah anakumbukwa zaidi wakati alipokutana na Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi ambapo alifunga bao moja pindi timu hizo zilipofungana 1-1, Desemba 8, mwaka jana kisha marudiano Medeama kuchapwa 3-0, Desemba 20, 2023.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Ghana, Sowah aliifungia Medeama bao hilo kwa mkwaju wa penalti dakika ya 27 kisha Pacome Zouzoua kuisawazishia Yanga huku mechi ya marudiano jijini Dar es Salaam nyota huyo alionyeshwa kadi nyekundu.

Taarifa za ndani zinasema chanzo cha maamuzi ya mabosi hao ni kutoridhishwa na namba zao za ufungaji katika michezo  waliyocheza msimu uliopita.

Na baada ya Simba kumchukua mshambuliaji Steven Mukwala raia wa Uganda, Yanga ilimfuatilia  na kuona jamaa sio mkali kumzidi Sowah ambaye anajua kufunga na ana nguvu za kupambana.

Yanga imewahi kukutana na Sowah msimu uliopita kwenye mechi mbili za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Medeama, mshambuliaji huyo akiwafunga Mabingwa hao kwa mikwaju wa penalti dakika ya 27, lakini Yanga walirudisha  kupitia kiungo wao Pacome Zouzoua, mechi hiyo ikiisha kwa bao 1-1.

Sowah aliwasumbua sana Yanga kwenye mechi hiyo, hatua ambayo ikawafanya mabosi wa timu kuendelea kufuatilia zaidi ingawa baadaye wakapunguza kasi baada ya kusajiliwa na timu nyingine dirisha dogo.

Yanga imepata taarifa kwamba Sowah ameachana na klabu yake ya Al-Nasr Benghazi ya Libya ambayo ameitumikia kwa miezi sita tu.

Sowah, ameandika barua ya kutaka kuachana na klabu yake na sasa akikamilisha mchakato huo tu atakuja nchini haraka kumalizana na Mabingwa hao mara tatu mfululizo Ligi Kuu Bara.

Sowah amezungumza na Mwanaspoti na kufunguka kuwa, amefuatwa na Yanga na wako kwenye hatua ya mwisho kumalizana akisema tangu alipokutana na klabu hiyo imebaki moyoni kwake.

“Bado tunaongea na viongozi wa Yanga, tunaelekea mwisho kabisa kuna mambo namalizana na klabu yangu, yakifikia mwisho nitakuja hapo Tanzania haraka, unajua tangu nilipokutana nao mashabiki wa timu hiyo wamebaki kwenye moyo wangu,”alisema Sowah.

Tangu ajiunge na Al-Nasr Benghazi dirisha dogo Sowah ameifungia mabao matano ambapo mchezo ambao aling’aa ni ule dhidi ya Al Hilal Benghaz aliofunga mabao manne peke yake wakati timu yake ikishinda kwa mabao 6-3.

Related Posts