Rombo. Mamia ya waombolezaji kutoka ndani na nje ya Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro wamefurika kwenye mazishi ya ndugu watatu kati ya wanne wa familia moja waliofariki kwa ajali ya gari wakitokea harusini mkoani Dar es Salaam kurudi nyumbani kwao Rombo.
Maziko ya wanafamilia hao yamefanyika leo Juni 28, 2024 katika makaburi ya familia yaliyopo katika Kijiji cha Samanga kilichopo wilayani Rombo.
Hata hivyo, vilio na simanzi vimetawala nyumbani hapo wakati miili hiyo ikiingizwa nyumbani hapo, ambapo waombolezaji waliokuwepo msibani hapo walishindwa kujizuia na kupiga ukunga wakati majeneza yenye miili hiyo ikiingizwa nyumbani hapo.
Ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia Jumatatu Juni 24, 2024, katika eneo la Bwiko, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, baada ya gari walilokuwa wakisafiria, aina ya Noah likitokea Dar es Salaam kuelekea Rombo kuacha njia na kupinduka na kusababisha vifo na majeruhi kadhaa waliokuwemo ndani ya gari hilo.
Waliofariki katika ajali hiyo ni mama mzazi wa bwana harusi, Cecilia Luka na dada yake, Antonio Luka pamoja na ndugu wawili wa bwana harusi ambao ni Godfrey Michael na Judith Michael, ambaye alizikwa Juni 25, 2024 wilayani Mwanga huku wengine wawili wa familia hiyo, Joshua Michael na Jackline Massawe (Michael) wakilazwa hospitali ya KCMC baada ya kuvunjika.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema ajali hiyo ilitokea Juni 24, 2024, alfajiri, katika eneo la Bwiko, Wilaya ya Korogwe na kueleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uchovu wa dereva na mwendokasi.
“Ni kweli tukio hili lilitokea eneo la Bwiko wilayani Korogwe, karibu na mpakani mwa Mkoa wa Kilimanjaro na Tanga, ikihusisha gari aina ya Noah ikitokea Dar es Salaam kuelekea Mkoa wa Kilimanjaro ambapo gari hilo lilikosa mwelekeo na kwenda pembezoni mwa barabara kisha kupinduka,” alisema.
Endelea kufuatilia mitandao ya Mwananchi kwa taarifa zaidi.