Mcameroon arejea Coastal Union | Mwanaspoti

COASTAL Union imeanza kusuka kikosi kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika, na tayari imemsainisha mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja, mshambuliaji Amza Moubarack kutoka Singida Black Stars.

Msimu uliomalizika hivi karibuni Amza alimaliza na mabao manne akiwa na Kagera Sugar aliyoichezea kwa mkopo akitokea Singida iliyokuwa ikiitwa Ihefu SC alikojiunga msimu wa 2022/23.

Siyo mara ya kwanza kwa Amza kukipiga Coastal, kwani aliichezea msimu wa 2021-2022 akitokea kwao Cameroon.

Taarifa kutoka ndani ya Wagosi wa Kaya zinasema tayari wamemalizana na Singida na mchezaji mwenyewe, hivyo msimu ujao atakuwa kikosi kwao.

“Kwa sasa mchezaji huyo yupo nchini kwao Cameroon anatarajia kurejea Tanzania Julai 10 kujiunga na wenzake,” kilisema chanzo chetu.

Mwanaspoti lilimtafuta Amza ili kuthibitisha taarifa hizo na hakutana kuzungumza mambo mengi akisema “Ni kweli, isipokuwa siwezi kulizungumzia hilo. Ukitaka maelezo mapana uliza timu hizo mbili Coastal na Singida.”

Related Posts