NYUMA YA PAZIA: Hakimi alivyokwepa kutoka jasho Ujerumani akakimbilia Arusha

NIMEMUONA Achraf Hakimi Mouh akizurura pale Arusha. Kuzurura? Hapana! Sio neno zuri hasa ukizingatia kwamba ametoa kiasi cha Sh1 bilioni kusaidia watoto wenye uhitaji katika kituo kimoja cha watoto wa aina hiyo pale Arusha.

Jana alitua Zanzibar. Hakimi amenikumbusha mbali. Amenikumbusha mambo mengi. Kwanza amenikumbusha pesa. Ndio, pesa ni sabuni ya roho. Pesa ni kila kitu, hasa kwa sisi ambao hatuna. Kelele zetu nyingi tulizielekeza kwa namna ambavyo taasisi yake imetoa Sh1 bilioni kama msaada kwa watoto wale wa Arusha.

Ni kweli, mfuko wake wa kusaidia mambo mbalimbali huwa unakusanya pia pesa kutoka kwa watu mbalimbali. Lakini hata kama Hakimi angeamua kutoa pesa mfukoni kwake, bado isingemsumbua. Ni mshahara wake wa siku kumi tu pale PSG. Ni mchezaji wa pili kwa kulipwa pesa nyingi katika soka la Ufaransa.

Analipwa Pauni 236,000 kwa wiki ambazo ni sawa au zaidi ya Sh800 milioni. Ukiongezea na vipesa vya siku chache za mbele anajikuta anaweza kutoa msaada wa shilingi za Kitanzania bilioni moja kwa mshahara wa siku kumi.

Lakini kama bado una njaa unawezaje kutoa kiasi hicho cha pesa wakati mshahara wako wa mwaka ni mdogo kuliko kiasi hicho? Huku kwetu Afrika wengi wameanzisha mifuko kama hii kwa ajili ya kutega pesa za wafadhili halafu wazitie katika matumbo yao. Hazipo sana katika kusaidia jamii.

Sasa unawezaje kudai kwamba Hakimi ameanzisha mfuko kwa sababu hiyo wakati pesa kama aliyowapa watoto wetu pale Arusha angeweza kuitoa mfukoni mwake kwa mshahara wa wiki moja tu kati ya wiki 52 ambazo zipo mbele yake? Hiyo ni achilia mbali kwamba ana mikataba yake mingi binafsi ambayo inamlipa pesa nyingi.

Papo hapo Hakimi akanikumbusha ni kwanini hayupo Ujerumani na yupo Zanzibar. Angeweza kuwa katika hoteli moja ya kifahari pale Ujerumani akiwa ni beki wa kulia wa kudumu katika kikosi cha Hispania. Lakini yupo Zanzibar akirandaranda kama mtalii akitokea Morocco.

Hakimi alizaliwa Madrid mwishoni mwa mwaka 1998. Ilikuwa Novemba. Moja kwa moja alikuwa anafuzu kucheza katika kikosi cha Hispania. Taifa ambalo amezaliwa. Wangapi tumewaona wakifanya hivyo? Lakini aliamua kucheza kwao Morocco.

Waarabu wana staili fulani ya maisha yao. Wanaweza kuishi London kama vile wapo Casablanca. Wanaweza kuishi Milan kama vile wapo Tunisia. Wanaishi katika tamaduni zao. Wakubwa wanarithisha watoto kuishi vilevile kama vile wapo katika mitaa ya Rabat.

Ukimuona mama yake Hakimi unajua wazi kwamba ni mama wa Kiarabu wa tamaduni za Morocco. Ushungi wake uko palepale. Staha yake iko palepale. Ndio maana hawa kina Hakimi, Riyad Mahrez, Soufiane Amrabat na wengineo walizaliwa Ulaya wakaamua kucheza katika mataifa ya wazazi wao Afrika Kaskazini.

Hakimi hakuwa mnafiki. Alianza kucheza katika kikosi cha Morocco chini ya umri wa miaka 17. Kuna wachezaji ambao huwa wanabadili gia angani. Huwa wanaanza na timu za taifa za vijana Wazungu, lakini kadri siku zinavyosogea na kuona hawana matumaini ya kucheza timu za wakubwa huwa wanabadili gia angani na kutaka kucheza timu za taifa za Afrika.

Hakimi na wazazi wake hawakutaka kuwa wanafiki. Licha ya ubora wake mwingi, lakini alianza kuichezea timu ya taifa ya vijana ya Morocco chini ya umri wa miaka 17. Hata kama angeamua baadaye kucheza timu ya wakubwa ya Hispania ni beki gani wa kulia ambaye angemweka benchi? Dani Carvajal? Hapana.

Kama angeamua kuichezea Hispania, basi leo Hakimi asingekuwa ametua Zanzibar akitokea Arusha. Angekuwa miongoni mwa mastaa wa Hispania ambao wangekuwa na uhakika wa namba kuanza pambano la kesho kati ya Hispania na Georgia.

Hakimi pia amenikumbusha mambo mengi. Bahati ya kuzaliwa Ulaya. Bahati hii inakubadili kiakili tangu ukiwa tumboni mwa mama yako hadi ukiwa mkubwa. Nilimuona Arusha akiwa na umbo kubwa kama alivyo. Ametimiza malengo mengi maishani.

Fikiria pia kama kina Nsajigwa Shadrack na Shomari Kapombe wangezaliwa Ulaya. Vipaji walivyopewa wangeweza kufika mbali zaidi. Matunzo mema kuanzia nyumbani, lishe bora, matunzo mazuri katika soka la utotoni Real Madrid na mambo mengineyo. Wangeweza kufika mbali zaidi na pengine kuwa zaidi ya Hakimi.

Hakimi pia amenikumbusha jambo jingine. Kwanini hatuwaheshimu wachezaji wetu wa timu ya taifa ya Tanzania? Majuzi nilikuwa Ivory Coast katika michuano ya Mataifa ya Afrika. Hawa ndio wachezaji ambao walikuwa wanakabiliana nao. Wachezaji walioandaliwa kwa kila kitu.

Kuna mchezaji wa Tanzania ameandaliwa kama Hakimi? Kwamba amezaliwa Madrid na anacheza soka katika kiwango cha juu kama yeye?  Hapana. Kuna mchezaji wa Tanzania anayeweza kutoa kiasi cha shilingi bilioni moja katika mfuko wake wa kusaidia watu? Hata Mbwana Samatta hawezi.

Wachezaji wetu wengi ambao wanaiwakilisha timu ya taifa wanacheza nyumbani, lakini nyakati hizi ambao wanakabiliana na kina Hakimi huwa wanajaribu kuziba pengo kubwa lililopo baina ya wao na sisi. Bado kama hatupati matokeo mazuri huwa tunalalamika.

Labda ni wakati wa kuwashukuru zaidi wachezaji wetu kuliko kulalama kila wakati. Pengo lililopo ni kubwa lakini hatutaki kuliona. Huwa tunajiangalia zaidi na ligi yetu ya Bara kuliko kuangalia ukweli uliopo kwamba pengo baina ya hawa walioandaliwa vyema na sisi ni kubwa. Kila la heri kwa Hakimi katika likizo yake ya Tanzania.

Related Posts