Bukoba. Watu tisa wamefikishwa mahakamani wakishtakiwa kwa kosa la mauaji ya kukusudia ya Asimwe Novath (2), mtoto mwenye ualbino akiwamo Paroko Paroko Msaidizi Elipidius Rwegashora wa Parokia ya Bagandika wilayani Misenyi Mkoa wa Kagera.
Washtakiwa hao wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba na kusomewa shtaka la mauaji ya kukusudia ya mtoto huyo.
Asimwe aliporwa kutoka kwa mama yake Mei 30, 2024 na watu wawili wasiojulikana nyumbani kwao saa 2.30 usiku katika Kitongoji cha Mbale, Kijiji cha Bulamula Kata ya Kamachumu wilayani Muleba.
Juni 17, 2024 mwili wa Asimwe ulipatikana ukiwa umetelekezwa kwenye mfuko wa sandarusi chini ya kalavati, kwenye barabara ya Ruhanga Makongora, kwenye kitongoji cha Malele kata Ruhanga. Juni 18, 2024 alizikwa nyumbani kwao.
Washtakiwa wamefikishwa mahakamani leo Ijumaa Juni 28, 2024 ambako Jamhuri imefungua shauri la mauaji ya kukusudia namba 17740 la mwaka 2024.
Washtakiwa wamesomewa mashtaka na Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Kagera, Waziri Magumbo mbele ya Hakimu Mkazi, Eliapokea Wilson.
Mshtakiwa namba moja katika kesi hiyo ni Elipidius Rwegoshora, ambaye watuhumiwa walipokamatwa na Jeshi la Polisi alitajwa kuwa ni Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bugandika.
Mshitakiwa wa pili ni Novath Venant, ambaye kwa mujibu wa ripoti ya Polisi ni baba mzazi wa Asimwe.
Wastakiwa wengine ni Nurdini Masudi, Ramadhani Selestine, Rweyangira Alphonce, Dastan Bruchard, Faswiu Athuman, Gozbert Alikad na Desdery Everigist, wote wakazi wa wilayani Muleba, mkoani Kagera.
Magumbo baada ya kuwasomea mashtaka alidai Mahakama hiyo haina mamlaka kisheria ya kusikiliza shauri hilo, hivyo washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote mpaka watakapofikishwa Mahakama Kuu.
Hakimu ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 12, 2024 shauri litakapotajwa, washtakiwa wote tisa wamepelekwa rumande katika Gereza la Wilaya ya Bukoba.