Rais Samia mgeni rasmi kilele maadhimisho ya kupinga dawa za kulevya

Mwanza. Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kufunga kilele cha maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya jijini hapa, filamu mbalimbali zitatumika kuonyesha athari ya matumizi ya dawa hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Juni 28, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema maadhimisho hayo yanayoanza leo katika Uwanja wa Nyamagana, kilele chake kitakuwa Juni 30, 2024 ambapo Rais Samia atahutubia wananchi kuhusiana na athari ya dawa hizo pamoja na jitihada za Serikali katika kupambana na matumizi yake.

“Juni 30, 2024 ndiyo itakuwa kilele cha shughuli hii wananchi wajitokeze kwa wingi ili Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) apate fursa ya kuzungumza na nao  katika kilele cha maadhimisho ya siku hii,” amesema Mtanda.

Ameongeza kuwa katika maadhimisho hayo yanayofanyika Juni ya kila mwaka, kutakuwa na kongamano la kitaifa juu ya matumizi ya dawa za kulevya nchini litakalofanyika katika ukumbi wa ofisi yake Juni 29, 2024 pamoja na filamu zitakazoonyesha athari za dawa hizo na namna Serikali inavyopambana kuzitokomeza.

“Washiriki wataona mambo mengi ikiwemo filamu zinazoonyesha mambo yanayoendelea na namna Serikali inavyokabiliana na dawa za kulevya,” amesema Mtanda.

Amesema pia wananchi watapata fursa ya kuelimika kuhusu dawa ya kulevya katika mabanda yatakayotoa elimu kwa siku tatu mfululizo, akiwataka wajitokeze kwa wingi.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Wekeza kwenye kinga na tiba dhidi ya dawa za kulevya”.

Mkazi wa Jiji la Mwanza, Rosalia Mgeta ameshauri katika maadhimisho hayo, Serikali iweke wazi watu waliochukuliwa hatua kwa makosa ya kujihusisha na dawa hizo kwa kuingiza au kusambaza nchini ili liwe somo kwa wengine wanaofanya biashara hiyo.

“Vijana wetu wanaharibika sana…dawa zinawaharibu sana kisaikolojia, kiakili, kimwili na hata kiuchumi. Naomba Serikali ianze kupambana na wanaoleta hivi vitu nchini kuharibu watoto wetu,” amesema.

Related Posts