Morogoro. Katika kuhakikisha utendaji unakwenda kwa kasi ya sayansi na teknolojia, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amemuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya Gairo, Sharifa Yusuph kuwanunulia madiwani wote vishikwambi.
Malima amesema lengo la vishikwambi hivyo ni kupunguza gharama za matumizi ya karatasi ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi kwenye halmashauri hiyo.
Malima ameyasema hayo leo Juni 28, 2024 wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani katika halmashauri ya Gairo kilichoketi kwa ajili ya kujadili hoja mbalimbali zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Amesema madiwani wanatakiwa kuwa na vishikwambi hivyo vitakavyowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa wakati na kwa haraka.
“Mkurugenzi, nakuagiza uhakikishe madiwani wote wawe na vishikwambi ili kupunguza gharama za kutumia karatasi kwa kiasi kikubwa, lakini pia jambo litakalorahisisha utendaji wa kazi za kila siku kwa ustawi wa halmashauri yenu kwa kuwa dunia ya leo inakwenda sambamba na ukuaji wa teknolojia.
“Ifikapo Septemba 30, 2024, vishikwambi vya madiwani wote viwe vimenunuliwa na kuanzia wakati huo msikae kikao chochote bila kuwa na simu hizo kwa kuwa mabaraza ya madiwani kwenye maeneo mengine wanatumia teknolojia katika vikao vyao, sasa kwa nini nyie mshindwe,” amesema Malima.
Kwa upande wake Yusuph alimuahidi mkuu huyo wa mkoa kutekeleza agizo hilo la kwamba madiwani watabadilika na wataacha matumizi ya karatasi.
“Ni kweli, kwenye vikao vyetu vyote tumekuwa tukitumia karatasi kwa ajili ya kusambaza nyaraka kwa madiwani, lakini agizo la mkuu wetu wa mkoa la kununuliwa kwa vishikwambi litafanyiwa kazi na tutahakikisha kama Gairo tunaenda sambamba na ukuaji wa teknolojia ili tuwe mfano wa kuigwa kwa halmashauri zingine hapa nchini.
Diwani wa Kata ya Kibedya, Masatu Butindi amesema iwapo madiwani watanunuliwa vishikwambi hivyo, itachochea utendaji kazi sambamba na utunzaji wa mazingira.
Diwani wa Kata ya Ukwamani Gairo,Frank Mbaigwa amesema Vishikwambi vitasaidia kujenga uelewa kwenye matumizi ya teknolojia kwa kuwa walio wengi walizoea matumizi ya karatasi jambo ambalo ni hatari kwa uchafuzi wa mazingira.