Serikali, mabalozi kukutana kujadili changamoto za uwekezaji

Dar es Salaam. Wakati mabalozi wanaowakilisha mataifa yao Tanzania wameomba kukutana na Serikali kujadili changamoto zinazowakabili wawekezaji wa kigeni, Serikali imesema imelichukua suala hilo kwa umuhimu wa kipekee.

Katika barua ya Juni 26, 2024, kwenda kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, mabalozi hao wamesema licha ya ongezeko la usajili wa biashara kutoka Dola bilioni 3 za Marekani mwaka 2022 hadi Dola 5.5 bilioni mwaka 2023, wawekezaji wanakumbana na vikwazo vikubwa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mabalozi hao kutoka Uingereza, Marekani, Uholanzi, Ireland, Ufaransa, Ubelgiji, Canada, Korea, Sweden na Ujerumani, wamezungumzia pia ukaguzi wa mara kwa mara unaofanywa kwa kampuni za kigeni nchini.

Waziri Makamba kupitia barua ya Juni 27, 2024, amesema ombi la mabalozi hao limekubaliwa ili kujadili changamoto zilizowasilishwa.

“Nitahakikisha waliotajwa wanashiriki katika mkutano huo ili uwe na tija. Nawasihi wawekezaji wanaotajwa kuandaa maelezo yanayofafanua kwa kina malalamiko yao,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.

“Pindi ripoti hiyo itakapowasilishwa kwetu, ndipo tutakapopanga mkutano kama mlivyoomba. Nipo tayari kuwaalika wawakilishi wao kuhudhuria mkutano wetu ili tuweze kusikiliza moja kwa moja kutoka kwao,” anaeleza Makamba katika majibu yake.

Kwa mujibu wa barua ya mabalozi, mbali na Makamba, wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo ni  Waziri wa Fedha, Waziri wa Uwekezaji na Mipango, Waziri wa Biashara na Viwanda, na Kamishna Mkuu wa TRA.

Waziri Makamba anasisitiza katika barua kuwa, Serikali ya Tanzania inazingatia utawala bora na kuheshimu sheria kama nguzo muhimu ya maendeleo na ustawi.

“Tunaheshimu utawala wa kisiasa na kiuchumi ambao unavutia uwekezaji na kusaidia maendeleo ya sekta binafsi,” amesema.

Makamba anasisitiza kuwa, mafanikio ya kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) katika miaka ya hivi karibuni, kama ilivyotajwa katika barua ya mabalozi, yanathibitisha imani ya jamii ya uwekezaji duniani kuhusu Tanzania.

Amewahakikishia mabalozi kuwa Serikali inachukua kwa uzito mkubwa madai ya ukiukaji wa taratibu unaofanywa na taasisi za umma, kwani yanaweza kuhatarisha mafanikio ya biashara na sifa ya Tanzania kama kituo rafiki kwa uwekezaji.

“Ahadi yetu ya kulinda uwekezaji wote na kuhakikisha mafanikio yao ni imara,” inasema barua hiyo.

Kuthibitisha madai yao, mabalozi wamesisitiza katika barua yao kuwa kampuni za kigeni zinapokea notisi zisizo na ushahidi kutoka TRA zinazodai malipo na upatanisho wa akaunti uliorejeshwa nyuma kwa hadi miaka 15.

“Kampuni nyingi zinakumbana na notisi za namna hiyo ambazo zinasimamisha akaunti, kusitisha shughuli, na kuathiri mishahara ya wafanyakazi na mtiririko wa fedha za watoa huduma,” inasema barua hiyo.

Mabalozi wanaripoti kuwa, kampuni licha ya kusaini mikataba ya msamaha wa kodi na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na wizara za kisekta, wamepewa taarifa na TRA kwamba mikataba hiyo haikubaliki kwa sababu haikutangazwa kwenye gazeti la Serikali.

Pia, wanaeleza TRA inatoza bili za kodi zisizokuwa na msingi wa sheria za Tanzania, na kuwatishia wawekezaji na washirika wao wanapopinga au kukata rufaa dhidi ya hali hiyo, na kufungia au kutaifisha akaunti za benki na mali za kampuni bila taarifa wala kufuata matakwa ya kisheria.

Kuhusu ukaguzi mara kwa mara, mabalozi wanasema hesabu za kampuni zinakaguliwa na kampuni kubwa za ukaguzi za kimataifa zilizoidhinishwa na Serikali ya Tanzania kuhakikisha zinazingatia viwango vya kimataifa.

Hata hivyo, wanadai ukaguzi wa pili na uchunguzi wa ndani unaofanywa na TRA unaleta hisia ya ukaguzi maradufu.

Licha ya taratibu hizo, mabalozi wanasema kampuni zinapokea notisi za malipo ya juu ya kodi.

“Kwa mfano, kampuni moja ilipokea notisi ya Sh1.2 bilioni, iliyopaswa kulipwa ndani ya siku tatu za kazi kwa madai ya miaka 12 nyuma, iliyoambatana na vitisho vya kufungia akaunti zao za uendeshaji na kuchukuliwa kwa fedha zao,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Related Posts