Serikali yakiri upungufu wa maprofesa, yaanika mikakati kuukabili

Dar es Salaam. Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo amekiri kwamba kuna uhaba wa wahadhiri nchini, hata hivyo amesema Serikali imechukua jitihada za kuhakikisha wataalamu kutoka nje wanakuja nchini kutoa mafunzo.

Japo hakutoa takwimu ya upungufu uliopo wa wahadhiri nchini, Profesa Nombo amesema hatua nyingine ambayo Serikali imechukua ili uhaba huo usiathiri utoaji wa elimu na ufanyaji wa tafiti ni kutoa vibali tayari vya ajira kwa watumishi wanaohitajika.

Profesa Nombo ameyasema hayo Juni 27, 2024 wakati akizindua kongamano la 12 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kampasi ya Mloganzila.

“Ni kweli uhaba upo na Serikali inatekeleza jitihada mbalimbali kupunguza uhaba huo na uhaba utapungua kupitia ‘umataifishaji’ wa walimu na wataalamu wengine kutoka nchi mbalimbali kuja kushirikiana nasi kwenye utoaji wa elimu na ufanyaji wa tafiti,” amesema.

Profesa Nombo ameeleza hayo wakati akizungumzia nia ya Serikali kuandaa mazingira mazuri na rafiki kwa ajili ya vijana kusoma na kufanya kazi katika mazingira yanayovutia na kuhamasisha katika kazi ya ufundishaji na utafiti.

Ripoti ya mwaka 2017 ya Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) ilikuwa imebainisha uhaba wa wafanyakazi wa masomo katika taasisi za elimu ya juu nchini kuwa asilimia 44.

Ripoti hiyo ilibainisha kuwa asilimia 53 ya wafanyakazi wa ngazi za juu waliokuwa wakifundisha katika vyuo vikuu walikuwa wamestaafu na walikuwa wakifanya kazi kama wafanyakazi waliopewa mikataba.

Ikumbukwe kwamba Mbunge wa viti Maalumu, Dk Tea Ntala, akiwa bungeni Mei 2024, aliibua hoja hiyo akisema kwa sasa nchini kuna maprofesa 93, huku vyuo vilivyopo vikihitaji maprofesa 516.

“Kwa sasa nchini tunao maprofesa 93 ambao wakifika miaka 70 tunataka wastaafu huku wengine hamjawajenga. Nashauri tuongeze muda wa miaka ya kustaafu na tuhakikishe tunaongeza wengine kutoka nje ya nchi,” alidai Dk Ntala bila kutaja rejea aliyoitumia kutoa takwimu hizo.

Takwimu za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia zinaonyesha mwaka 2022, Tanzania ilikuwa na maprofesa 226, kati yao 163 walikuwa maprofesa washiriki na 63 maprofesa kamili.

Kwa mujibu wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), hadi kufikia 2020 kulikuwa na jumla ya wahadhiri 7,187 katika taasisi za vyuo vikuu.

Kati yao 4,863 walikuwa katika vyuo vikuu vya umma na 2,324 katika vyuo vikuu binafsi. Miongoni mwao, 5,088 ni wahadhiri wa kiume na 2,099 wanawake.

Wakati huohuo, uandikishaji wa wanafunzi umekuwa ukiongezeka kwa wastani wa asilimia 4.7 kwa mwaka kutoka wanafunzi 177,963 katika mwaka wa masomo 2017/18 hadi wanafunzi 206,305 mwaka 2020/21.

Kwa mujibu wa maelezo ya aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Profesa Sifuni Mchome, mwalimu mmoja anapaswa kufundisha wanafunzi 20 wa masomo ya sayansi ya jamii, mwalimu mmoja watoto 10 wa fani za ukandarasi na mwalimu mmoja kwa wanafunzi watano wa masomo ya udaktari.

Katika hatua nyingine, kupitia kongamano hilo, Profesa Nombo amewataka watafiti kuja na mapendekezo ya njia mpya kushughulikia magonjwa yasioambukiza ikiwemo ya afya ya akili, uzee, ajali, kisukari, magonjwa ya moyo na saratani.

Pia, Profesa Nombo amewataka watafiti hao kuja na mapendekezo ya namna ya kujenga na kuimarisha maadili kwa watoa huduma za afya nchini na matumizi ya teknolojia hasa akili mnemba.

“Ninapenda mfahamu Muhas kwa kushirikiana na Serikali ipo katika mkakati wa kuanzisha vituo vingine vya umahiri Kampasi ya Mloganzila ikiwepo awamu ya pili ya ujenzi wa kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu na Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Afya ya Kinywa. 

Ameongeza kuwa “Miundombinu hii pamoja na mingine itakayojengwa baadaye itawezesha Kampasi ya Muhas kuwa kitovu cha mafunzo ya ubobezi ya afya na sayansi shirikishi,”amesema.

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Muhas, Dk Harrison Mwakyembe amesema kongamano la mwaka huu ni la  kipekee kutokana na  kumuenzi Mkuu wa Kwanza wa Chuo hicho hayati Ali Hassan Mwinyi.

Mbali na hilo, amesema kongamano hilo ni muhimu kwa watafiti kutoa njia ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiafya.

 Makamu Mkuu wa Muhas, Profesa Appolinary Kamuhabwa amesema kwa miaka yote Muhas itaendelea kuwa kitovu cha kutegemewa cha kitaifa kwa matokeo ya tafiti za afya, kusaidia sera na miongozo, na kusaidia taasisi nyingine nchini.

“Hadi sasa, Chuo kina miradi ya utafiti inayofadhiliwa 150, kinafanya kazi na zaidi ya taasisi 100 za ndani ya nchi na kimataifa na kuzalisha kati ya machapisho ya kisayansi 450 na 500 katika majarida yenye hadhi ndani na kimataifa kila mwaka,”amesema.

Mtafiti kutoka Muhas, Dk Edward Mhina amesema tafiti mbalimbali zitawasilishwa kwenye kongamano hilo akieleza kuwa utafiti wake umebaini namna wajawazito wanavyokimbilia matumizi ya dawa.

Sababu kubwa ni dawa hizo kuwa karibu na mazingira yao, kuchukua muda mrefu hospitalini kupata huduma akipendekeza Serikali iweke nguvu kudhibiti matumizi holela ya dawa.

Related Posts