TAMASHA la ‘Simba Day’ mwaka huu litafanyika Agosti 3 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam badala ya Agosti 8 kama ambavyo imezoeleka kila msimu.
Tamasha hilo ambalo limekuwa maarufu nchini limepangwa kufanyika Agosti 3 kutokana na ratiba ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inayohusiana na mechi za Ngao ya Jamii itakayopigwa kati ya Agosti 8-11.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Ijuma, Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally amesema kutokana na kuwepo kwa michuano ya Ngao ya Jamii siku hiyo wameamua kurudisha siku nyuma.
“Kabla ya kilele chake kutatanguliwa na Wiki ya Simba itakayoanza Julai 24 ambayo itakuwa na matukio mbalimbali ya kijamii kama kuchangia damu na (watu) wenye mahitaji maalumu,” amesema.
“Katika siku hiyo kutakuwa na matukio makubwa ya burudani kabla ya kuanza mchezo wenyewe ambao tutautumia kutambulisha kikosi chetu kuelekea msimu wa Ligi 2024/25.”
Ahmed amesema ratiba ya TFF imewabana na ndicho kilichosababusha wafanye mabadiliko ya tukio hilo, kwani Agosti 8 kutakuwa na michuano ya Ngao ya Jamii.
Michuano hiyo ya Ngao ya Jamii itakayohusisha timu nne zilizomaliza nafasi nne za juu za Ligi Kuu Bara iliyomalizika hivi karibuni zikiwamo watetezi Simba, Yanga, Azam FC na Coastal Union.