TAMWA ZNZ, Idara ya Michezo WEMA, ZAFELA, GIZ na CYD Kuandaa Mtoto wa Afrika Marathon

 

-Ni katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa
Afrika Zanzibar

CHAMA
cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa
kushirikiana na Idara ya Michezo, Jumuiya ya Wanasheria Wanawake
Zanzibar (ZAFELA), Taasisi ya Maendeleo ya Mashirikiano ya Ujerumani
(GIZ) na Kituo cha Mijadala kwa Vijana (CYD), inatarajia kuadhimisha ya
siku ya kimataifa ya Mtoto wa Afrika tarehe 29 Juni 2024 kwa kuandaa
mashindano ya riadha kwa wanafunzi wa skuli mbalimbali za Zanzibar.

Maadhimisho
hayo yatawahusisha jumla ya washiriki 150 ambapo kati ya hao
watakaoshiriki mashindano ni wanafunzi 75 kutoka katika skuli za Unguja
ambazo zimeshajiandaa kushiriki mashindano hayo.

Tukio
hili muhimu ambalo linalenga kuhamasisha usawa wa kijinsia katika
michezo litawaleta pamoja wadau kutoka taasisi za kierikali na
zisizokuwa za kiserikali ikiwemo wanafunzi kutoka skuli mbalimbali za
Unguja, wanamichezo, walimu wa michezo, na wadau wote wa masuala ya
usawa wa kijinsia.

Maadhimisho
haya yanatoa fursa kwa wasichana kuonesha vipaji vyao na uwezo wao wa
kushiriki katika michezo mbalimbali, pamoja na kujadili changamoto na
vikwazo vinavyowazuia kushiriki katika michezo na kuhimiza uanzishwaji
wa madawati ya jinsia katika taasisi za michezo.

Mashindano
haya ya riadha yataanza saa 12 na nusu asubuhi, yakianzia maeneo ya
Forodhani na yataishia katika viwanja vya Mnazi Mmoja Zanzibar
yakishirikisha wanafunzi wa jinsia zote  kutoka skuli mbalimbali za
Unguja.

Kaulimbiu ya wadau katika maadhimisho ya mwaka huu ni Wakati ni sasa! Wekeza katika elimu na michezo kwa watoto wote”. Tukio
hili linatarajiwa kuleta mwamko na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa
kuwapa nafasi sawa watoto wote kushiriki katika michezo, bila kujali
jinsia zao. Mashindano hayo yatatoa washindi watatu zaidi wanawake na
watatu wanaume na kutambuliwa rasmi.  

Tunaamini
kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kuleta usawa wa kijinsia na
kuwawezesha watoto wa kike na wa kiume kujifunza stadi za maisha,
kujenga ujasiri, na kushirikiana kwa amani na kuheshimiana.

Tunawaalika
wanahabari, wazazi, walezi, na wananchi wote kujitokeza kwa wingi
kushuhudia na kuunga mkono tukio hili la kihistoria katika kukuza usawa
wa kijinsia na kuwawezesha watoto wote kufikia ndoto zao katika Nyanja
mbali mbali bila vizuizi vyovyote.

Imetolewa na Idara ya mawasiliano,

TAMWA ZNZ.

info@tamwaznz.or.tz 

www.tamwaznz.or.tz 

             

Related Posts