Tanzania kukutana na mabalozi 9 kutatua changamoto za kikodi

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imekubali ombi la Mabalozi wa nchi mbalimbali walioomba kikao cha kujadili kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa lengo la kukwamua changamoto zinazowakabili wawekezaji kutoka nchi zao. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Mabalozi walioomba kikao na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni pamoja na balozi wa Marekani, Uingereza, Uholanzi, Ufaransa, Ubelgiji, Canada, Korea, Sweden, na Ujerumani.

Mabalozi hao wameomba kikao hicho kutokana na madai kwamba kumekuwepo na usumbufu mkubwa kutoka kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa wawekezaji wa kigeni ambao wamekuwa wakifungiwa akaunti na kudaiwa kodi za miaka 15 iliyopita.

Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Michael Battle

Akijibu ombi hilo kupitia barua aliyoiandika jana tarehe 27 Juni 2024, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, alisema serikali ipo tayari kujadiliana na mabalozi hao kama walivyoomba, wakiamini kikao hicho kitakuwa na tija na kushughulikia changamoto zilizojitokeza.

“Nimekubali maombi yenu ya kikao kujadili changamoto mlizoziorodhesha na nitaandaa uwepo wa maafisa wa serikali kutoka taasisi husika kama mlivyoomba. Ili kikao kiwe na tija tunaomba wawekezaji mnaowazungumzia waje na vielelezo vya kina vya changamoto zinazowakabili,” alisema Waziri Makamba.

Aidha, Waziri Makamba amewahakikishia Mabalozi dhamira na nia dhabiti ya Serikali ya Awamu ya Sita kuendelea kuboresha mazingira ya kibiashara nchini, ili kuvutia uwekezaji kutoka nje (FDI) kama ambavyo imefanikiwa kufanya ndani ya muda mfupi kutoka uwekezaji wa Dola za Kimarekani bilioni 3 (Sh trilioni nane) mwaka 2022 mpaka Bilioni 5.5 (Sh 14.5 trilioni) mwaka 2023.

Mabalozi hao wamelalamikia nini?

Kwa mujibu wa barua ya umoja wa mabalozi hao iliyoandikwa tarehe 26 Juni 2024 kwenda kwa Waziri Makamba, wameeleza wasiwasi wao kuhusu changamoto za hivi karibuni na zinazoendelea kuwakabili wawekezaji wa kigeni nchini Tanzania, hasa kuhusiana na taratibu za usimamizi wa kodi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Balozi Uingereza nchini Tanzania, David Concar

Barua hiyo yenye kichwa cha habari “Kushughulikia changamoto za haraka wanazokumbana nazo wawekezaji wa kigeni nchini Tanzania”, wamesema mataifa yetu yamepiga hatua kubwa katika kuvutia na kupanua uwekezaji bora wa kimataifa nchini Tanzania katika miaka michache iliyopita.

Hata hivyo, wamesema wanaamini kazi nzuri inayofanywa na watu wengi kurejesha sifa ya Tanzania kuwa kivutio cha FDI sasa inadhoofishwa.

“Wawekezaji wetu wengi wanakutana na usumbufu kutokana na notisi zisizo na ushahidi kutoka kwa TRA zinazodai malipo ya kodi kwa kukagua akaunti kwa rekodi za hadi miaka 15.

“Biashara nyingi zimekabiliwa na taarifa za mawakala wa benki kufungia akaunti, kusimamisha shughuli na kuathiri vibaya mishahara ya wafanyakazi na mtiririko wa pesa za wasambazaji.

“Makampuni yamesaini mikataba ya unafuu wa kodi na Kituo cha Uwekezaji Tanzania na wizara husika, lakini sasa inaelezwa kuwa TRA haitatambua wala kuheshimu mikataba hiyo kwa sababu haijatangazwa kwenye gazeti la Dodoma.

Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Wiebe de Boer

“Wawekezaji pia wanaripoti kuwa mawakala wa TRA hutoza bili zisizo za kawaida za kodi zisizoungwa mkono na sheria za Tanzania, kutishia wawekezaji na washirika wa Tanzania wakati makampuni yanapopinga au kukata rufaa, na kufungia au kukamata akaunti za benki na mali za kampuni bila taarifa wala msaada wa kisheria kwa wakati,” imesema barua hiyo.

Wameandika kwamba kwa miaka mingi, kampuni hizi hukaguliwa  na kampuni kubwa za kimataifa zilizoidhinishwa na serikali ya Tanzania, ili kuhakikisha uzingatiaji wa viwango vya kimataifa vya ukaguzi; ukaguzi wa TRA na kaguzi hizo hufanyika kila baada ya miaka mmoja na mwili.

“Licha ya taratibu hizi, makampuni sasa yanapokea notisi na mahitaji ya ziada ya malipo ya kodi. Kwa mfano, kampuni moja ilipokea notisi ya TZS 1.2 bilioni, ikitaka ilipwe ndani ya siku tatu kutokana na kodi zilizokwepwa kulipwa katika miaka 12 iliyopita Hayo yanafanyika huku kukiwepo na tishio la kufungiwa akaunti zao na fedha kuchotwa. Kampuni ililazimika kusitisha karibu shughuli zote za biashara kushughulikia suala hilo,” imesema.

Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Nabil Hajlaoui

Imesema mwelekeo huo umesababisha idadi kubwa ya biashara kufilisika, mamia ya makampuni kupunguza au kusimamisha shughuli za biashara ili kutatua changamoto hiyo ambayo pia imesababisha wanahisa wa kigeni kusitisha uwekezaji nchini Tanzania.

“Tunaomba kwa heshima kubwa kukutana na wewe mwenyewe (Makamba), Waziri wa Fedha, Waziri wa Uwekezaji na Mipango, Waziri wa Viwanda na Biashara na Kamishna Mkuu wa TRA ili kujadili njia nzuri zaidi ya kusonga mbele.

“Tumedhamiria kufanya kazi kwa ushirikiano na serikali ya Tanzania katika kutafuta suluhu za changamoto hizi ambazo zinakuza na kujenga upya imani katika mazingira ya biashara ya Tanzania, kulingana na azma ya nchi ya kufikia ukuaji wa uchumi jumuishi,” wameandika.

Related Posts