Wananchi Mbeya wahaha kusaka maji usiku

Mbeya. Wananchi wa mitaa ya Mponzi, Sinde, Chaula na Makunguru jijini Mbeya wameendelea kusotea huduma ya maji kwa zaidi ya miezi miwili tangu kukatika kwake, huku wanawake wakielelezea hofu yao kiusalama wanapoamka usiku kutafuta huduma hiyo.

Huduma hiyo ambayo ilipotea tangu Machi 2024 kwa baadhi ya maeneo, haijarejea tena na kufanya wakazi wa maeneo hayo katika kata za Isanga, Ilemi na Ilolo kukosa maji na kusababisha adha kwa wananchi hao.

Kwa sasa wananchi wanalazimika kuamka kati ya saa 10 na 11 alfajiri kutafuta huduma hiyo ambapo kimbilio kubwa imebaki kuwa chanzo cha maji cha Afrika ambapo wengi hupata msaada hapo, wengine wakitumia ya visima vya kuchimba ambayo si salama kwa afya.

Hata hivyo, tangu Mwananchi Digital iliporipoti changamoto hiyo, Juni 10, 2024, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya Uwssa) walikiri uwapo wa tatizo hilo huku wakiahidi kufanyia kazi ikisema kwa sasa upo mgao.

Mwananchi imefika katika baadhi ya maeneo ambayo ni kimbilio kwa wananchi kupata maji ikiwamo chanzo cha maji Afrika na visimani na kushuhuhudia foleni ya wananchi wakiwamo watoto wadogo wakihangaika kupata huduma hiyo.

Akizungumza na Mwananchi Digital kuhusu hatma ya kurejea kwa huduma ya maji katika maeneo hayo, Ofisa Habari na Uhusiano wa Mbeya Uwssa, Neema Stanton amesema tayari maji yamerejea kwenye baadhi ya maeneo.

Hata hivyo, amebainisha kwamba licha ya kurejea kwa huduma hiyo, amekiri kwamba mitaa mingine kutokuwa na huduma hiyo kutokana na mgao unaoendelea kwa ratiba na kuahidi kuendelea kufuatilia ambapo hayajapatikana.

“Huduma imerejea japokuwa kuna baadhi ambao bado hawajaanza kupata kutokana na ratiba ya mgao katika maeneo yao, tunaendelea kufuatilia kwa karibu,” amesema Neema.

Wananchi jijini Mbeya wakichota maji katika kisima ambacho si rasmi kwa matumizi ya nyumbani kufuatia changamoto ya huduma hiyo iliyopotea kwa zaidi ya miezi miwili sasa. Picha na Saddam Sadick

Wakizungumza leo Juni 28, 2024, baadhi ya wananchi wamesema tangu kukatika maji Machi 2024, wamekuwa katika wakati mgumu ikiwamo kuamka nyakati za usiku wakisema hawajaona utekelezaji wa kaulimbiu ya “kumtua mama ndoo kichwani”.

Maria Mwasomola, mkazi wa Mtaa wa Magege, amesema kwa sasa wanakuwa na hofu ya kutekwa na vibaka kutokana na msoto wa maji wanaokutana nao katika kutafuta huduma hiyo muhimu, hivyo wanaiomba Serikali kusikia kilio chao.

“Maji yenyewe siyo salama, watu wanadumbukiza vifaa vichafu, muda mwingine foleni ni kubwa na hukauka hadi tunahofia majambazi kututeka hasa sisi wanawake, Serikali ituangalie namna tunavyoteseka,” amesema Maria.

Naye Sumai Kalasya ‘Mama Mwenyekiti’ amesema tangu Machi hakuna huduma hiyo na kwamba ile kauli ya kumtua mama ndoo kichwani haipo.

“Tangu Machi hatuna huduma ya maji, maisha yetu yapo hapa kwenye chanzo hiki cha Afrika, tunashukuru ishu ya umeme lakini kwa maji ni shida na hatuioni kauli ya ‘kumtua mama ndoo kichwani’,” amesema Mama Mwenyekiti.

Kwa upande wake, Beatha Mapunda amesema changamoto ya maji ni kubwa ambapo inawalazimu kuamka usiku kwenda kwa majirani wenye visima kupata huduma hiyo licha ya kuwekewa mabomba.

“Muda mwingine tunaenda saa 9 usiku kwa majirani wenye visima, sisi hapa nyumbani ni zaidi ya mieizi minne hatujapata maji licha ya mabomba kuwapo,” amesema Beatha.

Elia Joshua mkazi wa Sinde amesema pamoja na mgao unaotajwa kuwapo, lakini kero ni kubwa kwani maji yenyewe hutoka usiku na kwamba matumizi ya maji ya visima hayana usalama.

“Maji ya mgao yanakuja usiku, lakini hata haya tunayotumia ya visima si salama kwa ujumla tunapitia changamoto kubwa katika huduma ya maji” amesema Joshua.

Naye Joyce Saveja ambaye ni mjane amesema kero ya maji imekuwa kubwa kwani hata mgao hutokea usiku wa manane na kwamba Serikali iingilie kati kunusuru maisha ya wananchi.

“Nilijichanga kadri ya uwezo wangu kununua mabomba ya maji, lakini hakuna huduma kwa sasa, uzee wote huu nilionao na ujane wangu nahangaika kupata maji serikali itusaidie” amesema Joyce.

Diwani wa Kata ya Sinde, Fanuel Kyanula amekiri kuwapo tatizo kubwa la maji akieleza kuwa maji wanayotumia siyo rasmi kwa matumizi sahihi ya nyumbani badala yake ni kwenye kutumia kufua.

“Wananchi wako sahihi maji kata ya Sinde ni kubwa kwani hata mgawo huja kwa wiki au zaidi, maji tunayotumia ni kwenye vusima au chanzo cha Afrika, ambapo tunasubiri majibu ya vipimo kama yatakuwa salama kwa matumizi ya nyumbani,” amesema Kyanula.

Related Posts