Morogoro. Dereva bodaboda anayefahamika kwa jina la Charles Ngaga, amefariki dunia usiku wa kuamkia Juni 28, 2024 katika Mtaa wa Kiswanya A, Manispaa ya Morogoro baada ya kushindana na wenzake kunywa pombe kali, chupa tano kwa wakati mmoja, jambo lililosababisha kifo chake.
Mjumbe wa serikali ya mtaa huo, Mohamed Mkandawile amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema Ngaga alikuwa dereva bodaboda, na kwamba shindano la kunywa pombe kali bila kupumzika ndilo limeondoa uhai wake.
“Ni kweli Charles Ngaga amefariki dunia katika mtaa wetu na anadaiwa kufariki baada ya kunywa pombe. Ni mnywaji lakini kwenye tukio ni kwamba kulikua na mashindano ya kunywa pombe kati yake na bodaboda wenzake.
“Ni hizi pombe za kisasa zilizoko kwenye vikopo vya plastiki, waliweka mashindano kwamba Charles Ngaga anaweza kunywa pakiti hizo tano kwa mkupuo na akamaliza kwa ahadi ya kupewa fedha,” amesema.
Amesema kulikuwa na watu jirani na eneo lile, wakawasihi kwamba waache huo mchezo maana unywaji huo sio mzuri hata kidogo, wakakaidi.
Amesema marehemu alipomaliza kunywa hizo pombe akarudi kwenye kituo chao cha bodaboda baada ya dakika 30, marehemu akaanza kuishiwa nguvu.
Mkandawile amebainisha kwamba baada ya kuona hali hiyo, bodaboda wenzake wakamchukua kumrejesha nyumbani kwake akiwa na bodaboda yake.
“Bahati mbaya, wazazi wake hawakuwepo, kwa hivyo wakamuacha hapo, na hata wazazi wake waliporejea hawakujishughulisha naye, walimuacha kwa kuwa alikuwa na kawaida ya kunywa pombe, ilipofika usiku saa 7 akafariki dunia,” amesema.
Mkandawile anasema baada ya tukio hilo kutokea, wale bodaboda ambao walikuwa wakifanya mashindabo na Ngaga kunywa hizo pombe kali wamekimbia mtaa huo wakihofia kukamatwa ambapo serikali ya mtaa huo kwa kushirikiana na jeshi la polisi wanaendelea kuwatafuta.
kwa upande wake, baba wa marehemu, John Ngaga amesema amepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mtoto wake.
“Kama familia tumepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mwanangu, siwezi kujua kwamba mwanangu alikuwa na ugomvi na watu wengine ama la, siku za nyuma alikua anakunywa pombe kawaida lakini hizi alizokunywa zimeondoa uhai wake. Tulimtegemea kwa kuwa alikuwa msaada kwetu, lakini tunashukuru Mungu kwa kila jambo,” amesema.
Ameongeza kwamba maziko ya mtoto wao yatafanyika Juni 30, 2024 kwenye makaburi ya Mtaa wa Kiswanya A, Manispaa ya Morogoro,” amesema Mzee Ngaga.
Ignass Eliud, bodaboda anayefanya kazi zake eneo la Sabasaba, amesema enzi za uhai wa Charles, alikua mchapakazi asiye na makuu lakini utumiaji wa vinywaji vikali ndio umesababisha uhai wake kukatishwa.
“Namfahamu Charles kama bodaboda mwenzangu hapa na siku ya tukio ilitokea ubishani kwamba atakayemaliza pakti tano za pombe kali angejichukulia fedha taslimu Sh10,000, yeye alikunywa akamaliza hizo pombe na akachukua fedha alizoahidiwa.
“Kwa kuwa zile pombe zilikua kali, zilimuathiri sana tumboni na kukosa nguvu hadi kufariki, hivyo kama vijana, kuna la kujifunza japokuwa tunasikitika kuona mwenzetu amefariki katika mazingira hayo,” amesema.