Deni la Taifa la Sh1 trilioni lilivyoibua mjadala Zanzibar

Unguja. Mkutano wa 15 wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar umehitimishwa Juni 27, huku miongoni mwa hoja zilizotawala mjadala ikiwa kuhusu deni la Taifa la Sh1 trilioni.

Katika mkutano huo uliokaa vikao 30 kujadili bajeti za wizara 18, wajumbe wa baraza walijadili na kuipitisha bajeti ya Serikali yenye mapato na matumizi ya Sh5.1 trilioni.

Mbali ya deni la Taifa, hoja zingine zilizoibua mjadala ni kuhusu mifumo ya kusimamia mapato na changamoto ya kuingiza bidhaa Zanzibar kutoka Tanzania Bara.

Hoja nyingine ni juu ya  asilimia 10 ya makusanyo ya halmashauri inayotakiwa kutolewa kwa ajili ya kukopesha makundi maalumu, ujenzi wa barabara na uwanja wa ndege wa Pemba, changamoto ya maji, kukatika umeme, na mfumuko wa bei.

Pia, suala la bajeti ndogo zinazotolewa kwa baadhi ya wizara, ambapo  licha ya ufinyu huo bado fedha zinazotengwa hazitolewi hivyo kurudisha nyuma utekelezaji wa miradi inayopangwa.

Hoja nyingine ni bajeti ya Serikali kukosa vyanzo vipya vya mapato.

Mapato ya Serikali kwa mwaka 2024/25 yanakadiriwa kufikia Sh5.182 trilioni ikiwa ni ongezeko la Sh2.342 trilioni sawa na asilimia 54.81 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2023/24 ya Sh2.840 trilioni. Hii inaonyesha ukuaji wa asilimia 82.44.

Kutokana na hayo, Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi chini ya Mwenyekiti, Mwanaasha Khamis Juma iliisisitiza Serikali kuyafanyia kazi kwa upekee maeneo ambayo yalionekana kugusa hisia na michango mingi ya wawakilishi.

Wakichanga hoja hiyo baadhi ya wawakilishi walisema licha ya mikopo kuwa mizuri, kuna haja ya kuangalia na kuchukua ambayo ina masharti nafuu, wengine wakisema haina tija.

Hoja hiyo licha ya kujadiliwa barazani, iliibua mjadala nje ya Baraza, wadau wa maendeleo na wanasiasa wakikoleza mjadala huo.

Viongozi wakuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, akiwemo Mwenyekiti wake Taifa, Othman Masoud na Makamu wake Zanzibar, Ismail Jussa kwa nyakati tofauti walisema mikopo haina tija kwa Taifa, wakieleza Zanzibar ina uwezo wa kujiendesha kutegemea rasilimali zake bila kuingia kwenye mikopo.

ACT-Wazalendo wakieleza hayo, viongozi wa CCM kwa nyakati tofauti, akiwemo Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Dk Mohammed Dimwa alisema nchi inakopa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na mikopo hiyo ni kwa masilahi ya umma.

Akihitimisha mjadala barazani kwa kujibu hoja za wawakilishi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya alisema deni hilo bado ni himilivu na Serikali itaendelea kukopa kwani hakuna Taifa linaloweza kuendelea kwa kutegemea fedha zake za ndani.

Wachambuzi wa masuala ya uchumi na fedha walikuwa na mtazamo tofauti wakipinga na kukubaliana kukopa.

“Kukopa si jambo geni wala la ajabu katika mataifa haya yanayoendelea ila kinachoangaliwa uwezo wako, hata yule anayetoa mkopo hawezi kuutoa iwapo akiona hauna uwezo wa kurejesha kwa hiyo nadhani hili linaibua mjadala lakini sidhani kama imeshafikia hatua hiyo,” amesema Abubakar Suleman mtaalamu wa uchumi,

Mtaalamu wa masuala ya fedha, Sued Said kutoka Chuo Kikuu Zanzibar (ZU) amesema pamoja na kukopa lakini Taifa halipaswi kujielekeza zaidi kwenye mikopo badala yake liendelee kubuni vyanzo vyake vya mapato ili hata ikitokea wafadhili wameisitisha kusionekane athari kubwa.

Katika bajeti ya 2024/25, Serikali haikuja na vyanzo vipya vya mapato, sababu kubwa iliyotajwa na Waziri Dk Saada ni kwamba, wanataka kuimarisha mifumo ili kusimamia vyanzo vilivyopo ambavyo wanaamini vikisimamiwa vyema vinaweza kuleta tija kubwa.

Uwanja wa ndege Pemba, utalii

Ujenzi wa barabara hususani kisiwani Pemba na kukamilisha ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba viliibua mjadala, wachangiaji wakitaka ukamilishwe ili kukifungua kisiwa hicho.

Mwakilishi wa Ziwani, Suleiman Makame Haji alisema mipango ya kujenga uwanja huo imekuwapo kwa muda mrefu sasa lakini hawaoni kinachoendelea akisema inadumaza maendeleo na utalii wa kisiwa hicho.

“Ndege zote zinazokuja Zanzibar lazima zipite Pemba zije kutua Unguja kisha watalii waanze kurejeshwa Pemba. Huu ni mzunguko mkubwa inatakiwa ndege zote za kimataifa zishuke pale Pemba,” alisema.

Katika jambo hili Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Mohamed alisema tayari Serikali imeshaingia mkataba na kampuni za kujenga uwanja huo na kuanzia Julai mwaka huu huenda utekelezaji ukaanza.

Pia suala la kuimarisha na kuvitangaza vivutio vya utalii ili kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea Zanzibar ilikuwa moja ya hoja zilizojadiliwa na kuchangiwa katika mitazamo tofauti.

Ili kuimarisha utalii Zanzibar, Baraza la Wawakilishi lilisema Serikali inapaswa kuendelea kuimarisha miundombinu ya barabara, usafiri na huduma za afya.

Katika eneo hili la utalii licha ya kuchangia asilimia 30 ya pato la Taifa, wajumbe walisema bado kuna mapato mengi yanayopotea kwa sababu ya kutokuwa na mifumo thabiti.

Wakichangia hoja hiyo akiwemo mwakilishi wa Mtoni, Hussein Ibrahim Makungu alisema ipo haja Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Uhamiaji na Kamisheni ya Utalii kuwa na mfumo mmoja ambao utasomana ili wageni wanapofika watambulike ni wangapi na hoteli walizofikia na muda watakaoutumia.

Waziri Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga alikiri bado wizara haina takwimu sahihi za wageni wanaoingia Zanzibar kwa sababu ya mifumo.

Hata hivyo, Waziri Saada alisema jambo hilo linakwenda kupatiwa mwarobaini kwani tayari taasisi hizo zimeanza kuunganisha mifumo, jambo litakaloiwezesha ZRA kukusanya kila kodi inayotakiwa.

Wajumbe walitaka Serikali kusimamia mfumuko wa bei.

Kilimo cha umwagiliaji kiliguswa na wengi wakitaka ifike hatua sasa Zanzibar ijitegemee kwa mazao badala ya kuendelea kutegemea vyakula kutoka nje ya nchi hivyo ijikite katika kilimo cha umwagiliaji.

Uharibifu wa mazingira na changamoto za uchimbaji mchanga holela vilizungumzwa kwa hisia, huku Serikali ikisema tayari imeshatoa miongozo namna ya kusimamia jambo hilo kwa vibali maalumu vya uchimbaji mchanga.

Makusanyo kiduchu na uwezeshaji vijana kiuchumi  ni jambo lililochangiwa na wengi katika bajeti ya Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji.

Changamoto kubwa ilionekana asilimia 10 ya fedha za halmashauri zinazotakiwa kukopeswa kwa makundi maalumu, hazitolewi kwenda kwenye wizara husika chini ya wakala wa uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Wawakilishi walitaka kusimamia taratibu za kutoa fedha hizo kwa makundi yaliyokusudiwa pamoja na kuwajengea uwezo wa namna ya kuzitumia,  kuzirudisha kwa wakati ili ziwanufaishe na wengine wanaohitaji.

Kwa upande wa elimu, wajumbe walichangia kwa wingi kuhusu mtalaa mpya wa elimu kwa ngazi ya elimu ya maandalizi na msingi, hivyo kutakiwa vitabu ambavyo vipo katika hatua ya uchapaji kuhakikisha vinapatikana haraka ili  wanafunzi wavitumie.

Ujenzi holela, migogoro ya ardhi vilijadiliwa na wajumbe wengi hivyo Serikali ilishauriwa kuhakikisha inaandaa utaratibu mzuri kupunguza changamoto hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla akiahirisha mkutano huo Juni 27, 2024 alitoa msimamo wa Serikali katika hoja mbalimbali akiagiza wizara zinazohusika kuhakikisha changamoto zinazotajwa zinashughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi.

Hata hivyo, pamoja na kutoa maagizo alitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja ikiwemo mfumuko wa bei na kupanda kwa bidhaa za vyakula, akisema Serikali inaendelea kuchukua jitihada za makusudi kuwapunguzia gharama za ukali wa maisha wananchi.

Alisema uzoefu unaonyesha wafanyabiashara wana tabia ya kupandisha bei za bidhaa kiholela.

Aliutaka uongozi wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kulifuatilia kwa karibu suala la bei elekezi na kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria kwa kila atakayebainika kwenda kinyume cha agizo la Serikali.

“Serikali inawataka wafanyabiashara kuwa wazalendo kwa kutopandisha bei kiholela kwani kunasababisha ugumu wa maisha kwa wananchi wetu.”

Related Posts