Dripu inayopiga simu, kutuma ‘sms’ kuleta mapinduzi

Dar es Salaam. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamewezesha kuboresha huduma mbalimbali zikiwamo za hospitalini kwa wagonjwa na hasa waliolazwa.

Kutokana na umakini unaohitajika wa kufuatilia mwenendo wa dripu za maji au damu wanazotundikiwa wagonjwa, Godwin Justine mwanafunzi wa Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) amebuni dripu ya kielektroniki.

Dripu hiyo imewekwa ‘sensa’ iliyounganishwa katika mfumo maalumu hivyo kuwa na uwezo wa kutuma ujumbe mfupi wa maandishi na kupiga simu kwa wauguzi wa zamu pindi inapokaribia kuisha.

Kwa mujibu wa Justine, mwanafunzi wa Veta mkoani Dodoma, lengo la kutengeneza dripu hiyo ni kusaidia kukabiliana na uhaba wa wahudumu wa afya uliopo nchini na kurahisisha utoaji huduma.

Kwa mujibu wa taarifa za Serikali kwa sasa Tanzania inakabiliwa na upungufu wa takribani asilimia 65 ya watumishi wa kada ya afya katika vituo vya kutolea huduma.

Akizungumza na Mwananchi, Justine amesema uwepo wa dripu hizo katika vituo vya afya na hospitali utasaidia kuweka urahisi wa kutoa huduma kwa wagonjwa.

“Hii pia itaboresha utoaji wa huduma kwa wagonjwa, watakuwa wakipata huduma kwa wakati, hata wagonjwa wakiwa wengi wataweza kufikiwa na si kusubiri kwa muda mrefu,” amesema.

Amesema hiyo pia itasaidia utoaji wa huduma hasa kwa wagonjwa wasioweza kuinuka kuwafikiwa wahudumu wa afya ili wawasaidie.

Akieleza namna inavyofanya kazi amesema kupitia kifaa maalumu kinachowekwa kwenye dripu ya maji au damu na kuunganishwa na mfumo maalumu, ndiyo utakaokuwa na uwezo wa kutoa ujumbe kwa wahusika.

“Katika ufanyaji kazi wake damu au maji yakifikia wastani wa asilimia tano hutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa waliopo zamu kuwaambia kuwa mgonjwa fulani maji au damu imekaribia kuisha, ikifika asilimia mbili itapiga simu ya dharura kwa mhudumu mmoja isipopokewa itahamia kwa mwingine hadi mfumo utakapozimwa au mgonjwa kufikiwa,” amesema Justine.

Ikiwa ujumbe mfupi na simu hazikuzaa matunda, basi dripu hizo zitakapoisha kabisa taa maalumu zilizofungwa katika chumba cha wahudumu wa afya zitawaka ikiwa ni kuwakumbusha.

Amesema tangu kubuniwa kwa dripu ya kielekroniki tayari imefanyiwa majaribio katika moja ya kituo cha afya jijini Dodoma na kuonyesha manufaa.

Akizungumza mmoja wa watembeleaji wa maonyesho hayo, Nancy Mpauka amesema kuendelezwa kwa mfumo huo kutasaidia utoaji wa huduma kwa wagonjwa.

“Kuna wakati unaweza kuwa umelazwa ndugu wote wametoka, dripu imeisha, huna nguvu za kunyanyuka wala kumuita mhudumu au unaweza kuita ila sauti yako haiwezi kufika kutokana na wao kuwa mbali sasa vitu kama hivi ni msaada mkubwa,” amesema Nancy.

Luois Mwanauta, amesema ni vyema Serikali ikaangalia namna ya kuzifanyia uendelezaji bunifu mbalimbali zinazofanywa na wanafunzi ili kusaidia katika utoaji huduma.

“Siyo ziishie tu hapa kwenye maonyesho, ziboreshwe zionyeshe matokeo katika jamii kama ilivyokudiwa,” amesema Louis.

Related Posts