Ghazouani, mwenye umri wa miaka 67, mwanajeshi wa zamani wa ngazi ya juu, ameahidi kuharakisha uwekezaji ili kuchochoea uongezeko la bei na mahitaji ya bidhaa muhimu katika nchi hiyo yenye watu milioni tano, wengi wao wakiishi katika umaskini licha ya utajiri wake wa mafuta ya kisukuku na madini.
Soma pia: Rais wa Mauritania anatoa wito kwa mataifa ya Afrika Magharibi kushirikiana dhidi ya itikadi kali
Ghazouani ambaye alichaguliwa kwa muhula wa kwanza mwaka wa 2019, anatarajiwa na wengi kushinda uchaguzi wa leo kwa muhula wa pili kutokana na umaarufu wa chama tawala. Wachambuzi wanasema anaweza kushinda katika duru ya kwanza, ikizingatiwa migawanyiko ya upinzani na raslimali alizo nazo rais huyo. Ndiye rais wa sasa wa Umoja wa Afrika. Upigaji wa duru ya pili ya uchaguzi huenda ukafanyika Julai 14.
Wapinzani wake sita ni pamoja na mwanaharakati anayepinga utumwa Biram Dah Abeid, aliyemaliza wa pili mwaka wa 2019 na asilimia 18 ya kura, mwanasheria Id Mohameden M’Bareck, mchumi Mohamed Lemine El Mourtaji El Wafi na Hamadi Sidi El Mokhtar wa chama cha Tewassol.
Soma pia: Mauritania na Mali zatafuta suluhu mvutano wa mpakani
Watu milioni 2 wamesijiliwa kupiga kura. Masuala muhimu kwao yanajumuisha vita dhidi ya ufisadi na kutengenezwa nafasi za ajira kwa vijana. Matokeo ya mwanzo yanatarajiwa kutolewa Jumamosi jioni huku matokeo rasmi yakitangazwa Jumapili au Jumatatu.
Mauritania inajiweka kama mshirika wa kimkakati wa nchi za Magharibi katika kanda ambayo imekumbwa na mapinduzi na machafuko, lakini nchi hiyo inakemewa kwa ukiukaji wa haki za binaadamu.
Uchaguzi huo unafanyika katika mazingira ya wasiwasi ya kikanda, huku nchi jirani za Mauritania zikitiswa na mapinduzi ya kijeshi na machafuko ya itikadi kali. Mauritania, moja ya nchi imara zaidi katika kanda ya Sahel, inasifiwa kuwa mshirika muhimu wa Magharibi katika kudhibiti uhamiaji, na kupambana na itikadi kali na haijakumbwa na mashambulizi yoyote tangu 2011.
Mauritania ina utajiri wa maliasili kama vile madini ya chuma, shaba, zinki, fosfeti, dhahabu, mafuta na gesi asilia. Inatazamiwa kuwa mzalishaji wa gesi ifikapo mwisho wa mwaka huu, wakati utakapozinduliwa mradi wa gesi ya baharini wa Greater Tortue Ahmeyin unaoendeshwa na BP kwenye mpaka na Senegal.
afp, reuters