Hatima ya Guede yaibua makundi mawili Yanga

KUMEZUKA makundi mawili ndani ya Yanga juu ya hatima ya mshambuliaji Joseph Guede, huku kila moja likiwa na hoja zake kwamba jamaa abaki au apewe ‘thank you’.

Yanga inataka kuachana na washambuliaji wake wawili Kennedy Musonda na Guede, kisha zitafutwe mashine zingine ikiona kama jamaa hawajafanya makubwa ingawa wote wameitumikia timu hiyo kwa nyakati tofauti.

Mwanaspoti linajua hata Kocha Miguel Gamondi bado anataka kusalia na Guede kwa vile tayari gari limeshawaka, lakini viongozi wamemletea watu wa kazi mezani.

Wakati mabosi wa Yanga wanapigania saini ya mshambuliaji Jonathan Sowah wa Ghana, Guede akapigiwa hesabu za kukatwa lakini hatua hiyo ikakutana na upinzani.

Wanaotaka Guede afyekwe wanasisitiza na Musonda naye limkute hilohilo kwa kuwa washambuliaji hao wawili wameshindwa kufunga angalau mabao 10 kila mmoja wakiwa na kikosi hicho.

Guede ameifungia Yanga mabao sita kwenye ligi ndani ya nusu msimu uliopita aliosajiliwa wakati Musonda akifunga mabao matano msimu mzima wa Ligi Kuu Bara ambao Yanga ilitetea ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo.

Hata hivyo, Musonda amemzidi Guede katika anga la kimataifa kwa kuifungia Yanga mabao matatu katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika wakati mwenzake akiwa na moja.

Kundi la pili linalomtetea Guede linaona mshambuliaji huyo kama amefunga mabao sita kwenye nusu msimu, akipewa nafasi zaidi msimu ujao anaweza kufanya makubwa kwa namna ya usajili mzito ulivyofanyika.

Wanaomtetea Guede wakapata nguvu kubwa kutoka kwa kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi ambaye Mwanaspoti linafahamu kuwa ripoti yake imembakiza mshambuliaji huyo kwa sharti kwamba kama ataachwa awe amepatikana mtu ambaye hataleta mashaka kwenye kufunga.

Hatua rahisi kwa Yanga ni kwamba washambuliaji hao wawili wote mikataba yao imefikia mwisho ambapo maamuzi yoyote ya kuwabakisha yanahitaji mchakato wa kuwaongezea muda zaidi.

Related Posts