MKURUGENZI Mtendaji wa KenGold, Kenneth Mwakyusa Mwambungu amesema kwa sasa wanaendelea na zoezi la kuboresha timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, huku akiweka wazi watazingatia matakwa yote kutoka kwa benchi la ufundi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwambungu alisema licha ya ukimya uliopo ila wanaendelea na mikakati ya kuisuka timu hiyo huku lengo kubwa likiwa ni kutengeneza kikosi kitakacholeta ushindani katika mashindano mbalimbali hasa Ligi Kuu Bara.
“Tunaendelea na mchakato wa kupata wachezaji bora watakaotusaidia kwa sababu tunataka tufanye vizuri na kuleta ushindani kama tulivyofanya Championship, ukimya wetu usiwatishe mashabiki kwani mbele watafurahia watakachokiona,” alisema.
Mwambungu aliongeza, wachezaji wengi walioipandisha timu hiyo Ligi Kuu Bara wataendelea kubaki nao kwa msimu ujao, licha ya kukabiliwa na changamoto kubwa kutoka kwa klabu nyingine ambazo tayari zimeanza kuwafuata zikiwahitaji kuwasajili.
“Sisi KenGold sio kama timu nyingine zinavyofanya, eti kwa sababu tumepanda ndio tuwaache waliotupambania kututoa huku chini, tutaendelea kuwapambania kuwabakisha, ila ikitokea kwa bahati mbaya tukashindwana basi tutaachana kwa amani.”
Timu hiyo ambayo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Gipco FC, kisha kuitwa KenGold, ilimaliza Ligi ya Championship msimu uliopita ikiwa mabingwa baada ya kukusanya pointi 70 ikiungana na Pamba Jiji iliyomaliza ya pili kucheza Ligi Kuu Bara.
Tayari timu hiyo imefikia makubaliano ya kufundishwa na aliyekuwa kocha msaidizi wa Coastal Union, Fikiri Elias baada ya Jumanne Challe aliyeipandisha Ligi Kuu Bara kutoka Championship kukosa vigezo vya kusimamia benchi la ufundi akiwa kocha mkuu.