Kigogo Takukuru, wenzake walioachiwa huru warudishwa kortini

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania, imeamuru kusikilizwa upya kesi iliyokuwa ikimkabili mhasibu wa zamani wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Geofrey Gugai na wenzake watatu, walioachiwa huru Novemba 2021.

Katika kesi hiyo, waliyoachiwa huru na Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Gugai pekee alikabiliwa na mashtaka ya kuwa na mali zisizo na maelezo, zenye thamani ya Sh3.63 bilioni.

Hukumu ya kusikilizwa upya kwa kesi hiyo imetolewa jana Juni 28, 2024 na Jaji Musa Pomo wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam baada ya kusikiliza rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) dhidi ya Gugai na wenzake.

DPP aliwasilisha rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kupinga kuachiwa huru kwa Gugai na wenzake, George Makaramba na Leonard Aloyce ambao kwa ujumla walikuwa wakikabiliwa na mashtaka tofauti 40.

Katika hukumu, Jaji Pomo amesema kulikuwa na dosari za kisheria katika mwenendo wa shauri hilo ambao ulikiuka kifungu cha 234(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) ambao ulifanywa na Mahakama iliyosikiliza shauri.

Jaji amesema dosari hiyo imefanya mwenendo wa kesi kuanzia Septemba 16, 2021 baada ya kufanyika mabadiliko ya hati ya mashitaka, kuanzia tarehe hiyo kuwa batili hivyo kuufuta katika kumbukumbu.

“Nimefanya hivyo kwa kuwa hakuna hukumu halali inayoweza kutokana na mwenendo batili, hukumu hiyo naiweka kando. Athari za kubatilisha mwenendo na hukumu kulifanya kusiwe na rufaa halali mbele ya mahakama,” amesema Jaji.

“Kwa hiyo naitupa rufaa (iliyokatwa na DPP) na kuagiza kusikilizwa upya kwa kesi hii kuanzia pale hati ya mashitaka ilipobadilishwa yaani Septemba 16, 2021 na masharti yote ya kifungu 234(2) cha CPA ni lazima yazingatiwe,” amesema.

Novemba 16, 2017, Gugai na wenzake walifikishwa kortini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashtaka ya jinai 40 yakihusu kuwa na mali nyingi ambazo hazina maelezo zilipatikanaje.

Makosa mengine yaliangukia katika kugushi na utakatishaji fedha.

Kosa la kumiliki mali ambazo hazilingani na kipato chake na hazina maelezo zilipatikanaje, lilimhusu Gugai akidaiwa kati ya Januari 2005 na Desemba, 2015 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, akiwa mtumishi wa umma, alipatikana na mali hizo.

Gugai akiwa mtumishi wa Takukuru, alimiliki viwanja vyenye thamani ya Sh3.63 bilioni, ambavyo thamani yake hailingani na mapato yake halisi ya zaidi ya Sh852.183 milioni na alishindwa kutoa maelezo namna alivyozipata.

Katika kosa la kugushi, upande wa Jamhuri ulidai mshitakiwa wa kwanza aligushi nyaraka za makubaliano ya mauziano kuonyesha viwanja hivyo alikuwa ameviuza kwa watu mbalimbali katika Jiji la Dar es Salaam.

Shitaka la kugushi lilimhusisha pia mshitakiwa wa tatu, Leonard Aloyce, ambaye naye alihusishwa kama mmoja wa watu walionunua viwanja saba.

Shitaka la utakatishaji wa fedha liliwahusu washtakiwa wote watatu.

Katika kuthibitisha mashtaka, upande wa Jamhuri uliita mashahidi 42 na kuwasilisha vielelezo 48, huku upande wa utetezi, washitakiwa walijitetea wenyewe.

Kulingana na mwenendo wa kesi hiyo, mwisho wa kesi baada ya kusikiliza ushahidi wa utetezi na kuupima, iliona upande wa mashtaka ulikuwa umeshindwa kuthibitisha mashitaka katika viwango vinakubalika na hivyo kuacha mashaka.

Mahakama iliwaachia huru washitakiwa, uamuzi ambao haukumridhisha DPP aliyekata rufaa akiegemea sababu saba akisema mahakama ilikosea kisheria kuwaachia huru washtakiwa kwa maelezo mashitaka hayakuthibitishwa.

Aprili 24, 2023 rufaa ilipoitwa kwa ajili ya kusikilizwa, mwanasheria mwandamizi wa Serikali, Christian Joel alimwakilisha DPP wakati wajibu rufaa walitetewa na mawakili Alex Mgongolwa, Seni Malimi na Nduruma Majembe.

Jaji aliagiza rufaa isikilizwe kwa utaratibu wa kila upande kuwasilisha hoja zake kwa maandishi. Hata hivyo, wakati akiandaa hukumu, alibaini Septemba 16, 2021, upande wa Jamhuri ulifanya mabadiliko ya hati ya mashitaka.

Mashitaka kulingana na hati mpya, kulikuwa na mabadiliko ya tarehe na mwaka katika maelezo ya kosa kutoka Julai 1, 2007 hadi Agosti, 2016 kutoka maelezo ya awali ambayo ni kati ya Januari 2005 hadi Desemba, 2015.

Katika kosa la kwanza kwa mujibu wa hati ya mashitaka ilidaiwa kosa lilitendwa na mshitakiwa wa kwanza (Gugai) na pili kipato chake halali kilikuwa zaidi ya Sh901.284 milioni kutoka Sh852.183 milioni za hati ya mashitaka ya awali.

Jaji amesema baada ya kubadilisha hati ya mashitaka, mahakama iliendelea na kesi bila kwanza kuzingatia kifungu cha 234(2) hivyo akaamua kuifungua rufaa hiyo ili pande zote ziweze kuwasilisha hoja mbele ya mahakama juu ya dosari hiyo.

Alisema Novemba 12, 2023 pande zote zilifika mbele ya Msajili wa Mahakama na kukubaliana kuwasilisha hoja hizo Aprili 5, 2024 mbele ya Msajili huyo wa Mahakama Kuu na hilo lilifanyika.

Katika hoja zake, wakili wa Serikali, Estazia Wilson alikiri hati ya mashtaka ilibadilishwa Septemba 16, 2021 kuhusiana na shitaka la kwanza lililokuwa likimhusu mshtakiwa wa kwanza.

Hata hivyo, akaieleza mahakama kubadilishwa huko kwa hati ya mashitaka hakukiuka haki za wajibu rufaa kwa vile mabadiliko hayo hayakuongeza mambo mapya na washitakiwa walipewa haki ya kuwadodosa mashahidi.

Alijenga hoja kuwa kama mahakama itaona kifungu hicho cha 234(2) cha CPA kilikiukwa na kufanya mwenendo wa kesi uwe batili, basi ubatili huo unapaswa kuanzia pale hati ya mashitaka ilipobadilishwa, hivyo isikilizwe upya.

Wakili huyo alidai haitaupa nafasi upande wa Jamhuri kujaza mashimo ya mapungufu ya ushahidi wao na anaamini ushahidi ambao ulishapokewa unatosha kuwatia hatiani washtakiwa kwa makosa waliyoshitakiwa nayo.

Upande wa wajibu rufaa (Gugai na wenzake), walikiri kutozingatiwa kwa kifungu hicho cha sheria Septemba 16, 2021 Jamhuri ilipobadili hati ya mashitaka.

Ulieleza mahakama haikuwajulisha haki yao ya kuwaita tena mashahidi ambao walikuwa tayari walishatoa ushahidi wao kwa kuegemea hati ya mwanzo.

Hata hivyo, walikuwa na maoni kuwa dosari hiyo ya mahakama haikuathiri kwa vyovyote haki yao na kwamba, kwa mtizamo wao hilo haliwezi kufanya mwenendo wa shauri hilo usiwe sahihi kwani mwishoni, mahakama iliwaachia huru.

Walisema kama wangekuwa wametiwa hatiani, hapo ndiyo kungesemekana haki haikutendeka kwa mahakama kushindwa kuzingatia kifungu hicho cha 234(2) na kwamba wao wanaona rufaa hiyo ipo kihalali mbele ya mahakama hiyo.

Wajibu rufaa hao walijenga hoja kuwa kama mahakama itaona kuwa mwenendo wa shauri hilo haukuwa sawa, kusiamuriwe kusikilizwa upya kwa kesi baada ya kubatilishwa kwa mwenendo na kufutwa kwa hukumu ya kesi hiyo.

Katika hukumu Jaji amesema dosari hiyo imefanya mwenendo wa kesi kuanzia Septemba 16, 2021 baada ya kufanyika mabadiliko ya hati ya mashitaka uwe batili wote kuanzia tarehe hiyo na kuufuta wote pamoja na hukumu ya mahakama.

Related Posts