Arusha. Shule ya Ukunga na Uuguzi ya Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), imetoa elimu ya afya, mabadiliko ya tabianchi na huduma za vipimo bure kwa wananchi katika makundi mbalimbali mkoani hapa.
Hatua hiyo inalenga kuongeza imani na ubinadamu kwa wanafunzi wanaosomea ukunga na uuguzi kutoka AKU na kurudisha wanachokipata na kujifunza kwa jamii.
Akizungumza na Mwananchi leo Juni 29, 2024, Mhadhiri wa AKU, Dk Stewart Mbelwa amesema hatua hiyo ni utaratibu kwa wanafunzi wanaofanya shahada ya kwanza ya uuguzi na ukunga wanapokaribia kumaliza kutoa huduma za kijamii kama hizo.
Kabla ya kufanya shughuli hiyo, Dk Mbelwa amesema walifanya tathimini na kugundua matatizo ya afya akili na afya kwa ujumla yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi, ndiyo maana AKU imeamua kuingilia kati kwa lengo la kuwasaidia wananchi.
“Mwaka huu katika shughuli hii, tumejumuisha vitu vitatu vikiwamo afya ya jamii, afya akili na mabadiliko ya tabianchi yanavyoleta matokeo katika afya ya jamii. Tumekwenda katika soko la Ngaramtoni juu kutoa elimu ya afya kuhusu kujikinga na magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza,”amesema na kuongeza.
“Lakini tumepima bure afya za wananchi ikiwemo uzito, sukari na presha na wale waliobainika kuwa na changamoto tumewapa rufaa kwenda hospitali kwa matibabu zaidi na waliohitaji huduma za ushauri tuliwapa pia,” amesema Dk Mbelwa.
Kwa mujibu wa Dk Mbelwa, shughuli ilihusisha timu ya wanafunzi 49 wa AKU na walimu wawili, lakini pia walishirikiana na AKU tawi la Arusha.
“Kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wananchi wakiwemo wateja waliokuja sokoni kwa ajili ya kufanya ununuzi, ambapo walitumia fursa hiyo kupata ushauri, huduma za afya na vipimo bure. Tulianza asubuhi hadi saa 12 jioni,” amesema.
Dk Mbelwa amesema mabadiliko ya tabianchi yana uhusiano mkubwa na tatizo la afya ya akili na afya kwa ujumla, akitolea mfano nyakati za kiangazi baadhi ya wafugaji walipoteza mifugo yao kwa kukosa chakula na maji hali iliyosababisha kuathirika kisaikolojia.
“Tulichokigundua, wafugaji wana chanzo kimoja cha maji ambayo ni mabwawa wanayotumia wanyama pori, mifugo na binadamu, pia hawana vyoo.
“Sasa wakati wa kiangazi mabwawa yanakauka na kupata changamoto, lakini wakati wa mvua yanajaa na kwa sababu hawana vyoo uchafu wote unakwenda katika mabwawa na kusababisha magonjwa,” amesema Dk Mbelwa.
Mkazi wa Arusha, Onesmo Mollel ameishukuru AKU kwa hatua ya kuwafuata wananchi katika maeneo ya masoko na kuwapata huduma za elimu ya afya na vipimo bure.
“Unajua baadhi yetu hatuna utaratibu wa kupima afya zetu, lakini fursa zinapotokea hasa umefuatwa katika eneo lako kazi lazima uchangamkie ili kuimarisha afya ya mwili tunaishukuru sana AKU,” amesema Mollel.
Mmoja wa wanafunzi wa AKU walioshiriki kutoa huduma hizo, Groly Mwankenja amesema: “Tumetoka katika mazingira ya hospitali tumekwenda kwenye jamii ili kuwasaidia wananchi na kujua magonjwa yanayowasumbua kwa lengo la kuwapatia vipimo na ushauri wa kiafya.
“Kuna baadhi ya watu wanaogopa kwenda hospitali, lakini ukiwafuata wanajisikia kama vile wapo nyumbani na wanatoa ushirikiano. AKU tumeamua kuchangamana na watu na kutoa elimu ya afya na vipimo, pamoja na ushauri bure, ”amesema.
Ameongeza: “Hii kwetu sisi kama wanafunzi imekuwa ni faraja kwani imetuwezesha kujua afya za wananchi, wanataka nini na kwa nini baadhi yao hawaendi kupima magonjwa yasiyoambukiza.”