Manula kuondoka Simba, Azam FC yatajwa

ALIYEKUWA kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula hatakuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo msimu ujao baada ya kurudi timu ya zamani ya Azam FC.

Kusajiliwa kwa Manula ni wazi kuwa ofa ya kipa namba mbili wa Yanga Abuutwalib Mshery aliyekuwa anatajwa kujiunga na timu hiyo limekufa.

Manula aliyeichezea Simba kwa mafanikio, amedumu kwa misimu saba, alitua klabuni hapo mwezi Agosti mwaka 2017, akitokea Azam.

Kipa huyo ambaye msimu ulioisha haukuwa mzuri kutokana na kusumbuliwa na jeraha la nyonga anatajwa kurudi Azam kwa msimu ujao akiungana na kipa namba moja wa timu hiyo aliyeongezwa mkataba Mohamed Mustafa ambaye alikuwa bora msimu ulioisha.

Chanzo cha kuaminika kutoka Azam, kimeliambia Mwanaspoti, muda wowote kuanzia sasa wanamalizana na kipa huyo ambaye wamekiri kuwa wanaamini atatoa ushindani kwa Mustafa aliyesajiliwa kaa mkopo kutoka Al Merrikh.

Azam msimu huu imeachana na Abdulai Iddrisu na Ali Ahamada wameondolewa katika usajili wa kikosi hicho baada ya kuonekana watakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na majeraha mbalimbali waliyoyapata mwaka jana.    

Iddrisu anauguza jeraha la bega lake la mkono wa kushoto alilofanyiwa upasuaji nchini Afrika Kusini sambamba na Ahamada anayesumbuliwa na goti la mguu wa kushoto.

Related Posts