Arusha. Watumishi wawili wa afya katika kituo cha Levolosi jijini Arusha wamesimamishwa kazi kwa muda usiojulikana kupisha uchunguzi wa tuhuma za uzembe kazini na kusababisha watoto watatu wa familia moja kufariki kwa ajali ya moto.
Rungu hilo limewaangukia watumishi hao Juni 28, 2024 baada ya tuhuma zilizoelekezwa kwao moja kwa moja na baadhi ya wananchi waliodai kuwawahisha watoto hao katika kituo hicho cha afya wakiwa wazima kwa matibabu, lakini uzembe wa wahudumu hao kutowachangamkia katika kuwapatia huduma kumesababisha vifo vyao.
Ajali hiyo ya moto iliyotokea Juni 22, 2024 katika eneo la Olmatejoo jijini Arusha, inayodaiwa kusababishwa na kompyuta mpakato (laptop) iliyokuwa imechomekwa kwenye soketi ya umeme, kushika moto na kuunguza kochi, ilisababisha vifo vya watu wanne ambao ni baba (Zuberi Msemo) na watoto wake watatu.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa jiji la Arusha, Mhandisi Juma Hamsini amesema, amewasimamisha kazi watumishi Fatma Mohamed Amir na Kamwana David ili kupisha uchunguzi wa madai ya kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Mhandisi Hamsini amesema amefikia uamuzi huo kutokana na taarifa ya mwananchi kulalamika kucheleweshwa kupatiwa huduma kwa wagonjwa watatu wa ajali ya moto waliofikishwa kituoni hapo Juni 22, 2024.
“Kutokana na hayo, nimeamua kuwasimamisha kazi; Fatma Mohamed Amir, aliyekuwa mapokezi siku hiyo, sambamba na Ofisa Tabibu, Kamwana David kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili,” amesema.
Pia, amesema wameunda timu ya kufuatilia kwa kina na kisha kuwasilisha ripoti hiyo ya uchunguzi kwa mwajiri.
“Lakini pia, nawasisitiza watumishi wengine kuzingatia weledi na maadili wanapotoa huduma kwa wananchi,” amesema mkurugenzi huyo.
Awali, mara baada ya kutokea kwa ajali ya moto, alfajiri ya Juni 22, 2024, majirani walifanikiwa kuwaokoa watoto watatu ambao ni Mariam Zuberi (9), Salma Zuberi (7) na Bisma Zuberi (3) na kuwawahisha katika kituo cha afya kilichoko karibu nao (Levolosi).
Wakizungumza na waandishi wa habari, majirani hao wamesema uzembe wa madaktari, ulichangia kwa kiasi kikubwa watoto hao kupoteza maisha.
“Nasema hivyo kwa sababu mimi nilimfikisha mtoto wa kwanza hospitali akiwa anapumua vizuri ingawa kwa kukoroma lakini dokta ananielekeza nimuweke kitandani nikafungue kwanza faili, nilipie ndio amhudumie,” anasema Kudra Seif na kuongeza:
“Wakati ananielekeza hivyo, ndio mtoto wa pili na wa tatu nao wakaletwa na watu wengine, wakaambiwa wawalaze kitandani, lakini anaendelea kusisitiza tufungue faili, mimi nilimjibu hawa watoto ni jirani zangu tu, nawasaidia sijui details zao, hivyo tunaomba msaada kwanza, aliitikia na kuondoka akisema anakwenda kutafuta mashine ya vipimo,” amesema.
Kudra amesema kuwa baada ya zaidi ya dakika 10, daktari yule alirudi bila mashine yenyewe na kumtuma mwenzake akalete na yeye kukaa kusubiri huku watoto wakizidi kukoroma wakiwa kitandani hadi kufa bila kupatiwa huduma yoyote ya kwanza wala vipimo.
“Tulishuhudia watoto wakiwa kitandani bila huduma hadi wanakata roho,” amesema Kudra.
Kudra amesimulia kwamba hata baada ya kuzembea na kusababisha vifo hivyo, wahudumu hao waligoma pia kuwasitiri watoto hao kwa kuwafunika mashuka na kuwataka kurudi nyumbani kuleta nguo za kuwafunika kwa ajili ya taratibu za kuhamishwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.
“Walishindwa hata kuwafunika mashuka, wanasema kaleteni shuka nyumbani, au leteni nguo zenu tuwafunike, tunaawaambia jinsi unavyotuona hatuna nguo za ziada, wanalazimisha basi rudini nyumbani kaleteni shuka muwafunike watoto, tukawaomba watupe shuka za hospitali tutarudisha lakini waligoma kabisa kuwasitiri,” amesema Kudra.
Mwanamke mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mama Nasra amesema kutokana na hali za watoto hao wakati wanawahishwa hospitali, wangepatiwa matibabu ya haraka ingeweza kuokoa maisha yao.
“Yaani wangewawahi kwa huduma ya kwanza si ajabu leo watoto wale wangekuwa hai, hawakuwa na majeraha yoyote zaidi ya kumeza moshi pekee, hawakujali wala kuthamini mgonjwa bali wao wanaangalia malipo kwanza, kiukweli imetusononesha sana,” amesema.