KUNA vitu vingine vinaendelea nchini vinashangaza sana. Ni kama hili sakata la usajili wa Clatous Chama. Ni jambo la kushangaza.
Huko mitandaoni kumechafuka. Huyu anasema Chama ni wa Simba mwingine anakuja anasema ni wa Yanga. Ni mkanganyiko mkubwa. Kwanini, subiri nitakwambia.
Chama alikuwa mchezaji wa Simba hadi msimu unamalizika. Amecheza Simba tangu 2018 ukiacha miezi sita aliyokwenda kupoteza pale RS Berkane ya Morocco.
Alikuwa mali ya Simba. Kwanini sasa wakati wa usajili Simba inaanza kugombania mchezaji wao na Yanga? Ni kama vile sasa watu wangekuwa wanasema Stephane Aziz Ki ni mali ya Simba. Yaani Yanga ingekuwa inagombania mchezaji wake na Simba.
Kwanini? Nitakwambia. Kuna kosa kubwa ambalo linafanywa na timu zetu kwa wachezaji wake. Kusubiri hadi mkataba unamalizika kabisa ndipo wanaanza mazungumzo.
Kimetokea kwa wachezaji wengi. Unakumbuka ya Haruna Niyonzima na Ibrahim Ajibu? Yalikuwa ni kituko kingine. Niyonzima alimaliza mkataba na Yanga. Kumbe bado walikuwa wanahitaji. Baada ya msimu ndipo wakaanza kuhangaika naye. Kumbe alishasaini Simba, akaenda zake.
Ajibu naye alimaliza mkataba na Simba. Hawakuona umuhimu wa kumpa mkataba mpya kabla msimu haujamalizika. Akasepa zake kwenda Yanga. Sinema ikaishia hapo.
Ni kama ilivyokuwa kwa Yanga na Fiston Mayele mwaka jana. Yanga waliacha Mayele akamaliza mkataba ndipo wakaanza kubanana naye asaini mkataba mpya.
Yaani mchezaji aliyefunga mabao 16 katika mwaka wake wa kwanza unaachaje kumwongeza mkataba? Ni ajabu. Matokeo yake Mayele akaondoka bure kwenda Pyramids ya Misri, akiwa kinara wa mabao kwa misimu miwili mfululizo. Msimu wake wa mwisho alifunga mabao 17 akiwa Mfungaji Bora na huko CAF alifunika pia na mabao 14, yakiwamo saba ya Kombe la Shirikisho Afrika yaliyompa tuzo ya Afrika.
Ni kama haya ya Aziz Ki pia. Hakua amepewa mkataba mpya hadi mwishoni mwa msimu. Akawa huru. Yanga wakaanza kuhaha. Matokeo yake wametoa fedha nyingi kupita kiasi kumbakisha. Anakua mchezaji ghali zaidi kwenye Ligi yetu.
Sasa turejee kwenye sakata la Chama. Simba walifahamu Chama anamaliza mkataba mwishoni mwa msimu. Wala hawakuhangaika kumpa mkataba mpya.
Baadhi ya watu wa Simba walianza maneno kuwa Chama amekwisha hivyo wamuache aende zake. Ni kweli Chama amekwisha? Sidhani. Ni maneno tu yalitengenezwa na baadaye yakageuzwa kuwa imani. Na baadhi ya Wanasimba wakaamini.
Nini kimetokea? Msimu ukamalizika na Chama hakua amepewa mkataba mpya. Simba wakakaa kimya na Chama naye akakaa kimya.
Zikapita wiki tatu hakuna mazungumzo kwa pande zote mbili. Ni ishara kuwa ndoa imevunjika. Hata kwenye mahusiano ya kimapenzi ukimya wa pande zote mbili kwa wiki tatu unatosha kabisa kuyavunja. Ndivyo ambavyo Hidaya aliachana na Romeo. Nitakupa hii simulizi siku nyingine.
Baada ya wiki tatu zikaja taarifa nyingi kuwa Chama amesaini Yanga. Presha ikawa kubwa kwa Wanasimba. Wakaanza kumtaka Mohamed Dewji ambakishe Chama wao. Inawezekanaje?
Clatous Chama. Mwamba wa Lusaka. Mchezaji Bora wa zama hizi kwenye Ligi yetu anamaliza msimu. Anakaa wiki tatu hana timu. Mmekaa kimya. Unadhani bado unaweza kumpata?
Simba wamerudi kwa kasi ya ajabu kuanza mazungumzo na Chama. Wanataka kumpa mkataba mpya. Yaani mchezaji alikua wako, unaanzaje kuhaha dakika za jioni kumpa mkataba mpya? Ni kichekesho.
Nadhani kama Simba walikua na mpango na Chama walipaswa kumalizana naye mapema. Haya wanayofanya sasa hata yeye anawashangaa. Alikua sebleni kwao, Leo wanaanza kumgombania na jirani.
Nina uhakika kuwa Chama ameshasaini timu nyingine. Hawezi kukaa muda wote bila kupata ofa nyingine. Ila acha tuone hii sinema itamalizika vipi.
Kwenye hili la kuongeza mikataba wachezaji kwa wakati nawakubali Azam FC. Wakisharidhika na mchezaji wanamwongeza kifungo mapema. Ndio maana hata kuondoka kwa Prince Dube ikawa shida. Azam walishampa mkataba mpya mapema. Ili kuondoka imebidi alipe fedha za maana.
Wachezaji wote muhimu pale Chamazi huwa hawaachwi wamalize mikataba. Ndio weledi wenyewe ulivyo.