Sekta ya elimu hatarini | Mwananchi

Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imekiri kuwashikilia watu 17 wanaotuhumiwa kuwafanyia mitihani wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), ikielezwa waliahidiwa malipo ya kati ya Sh30,000 na Sh50,000 kwa kila mtihani.

Mbali na watuhumiwa hao, limethibitisha kuwashikilia wanafunzi saba wanaodaiwa kuwa ndiyo waliokuwa wakifanyiwa mitihani hiyo, huku wengine 10 wakiendelea kusakwa.

Tukio hilo linaongeza idadi ya ambayo yamewahi kuripotiwa ya udanganyifu kwenye mitihani katika ngazi ya elimu ya msingi na sekondari, hivyo kuiweka katika hatari sekta ya elimu kupata wahitimu wasio na sifa.

Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) linapotangaza matokeo, mara kadhaa limekuwa likieleza kuwapo kwa matukio ya udanganyifu katika mitihani, hata kufikia hatua ya kuvifungia vituo vya mitihani.

Januari 25, 2024 wakati akitangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne Katibu Mtendaji wa Necta,  alieleza baraza hilo kufuta  matokeo ya watahiniwa 102 baada ya kubainika kuwa walifanya udanganyifu kwenye mtihani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Elifas Bisanda watuhumiwa walikamatwa kuanzia Juni 18, 2024 katika vituo vya Ilala na Kinondoni wakiwa na vitambulisho vya kughushi na tiketi ya ukumbi wa mitihani.

Akizungumza na Mwananchi, jana Kaimu Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, SACP Foka Dinya alisema watuhumiwa 17 wako chini ya ulinzi katika Kituo cha Polisi Oysterbay, Kinondoni.

“Wale waliokuwa wanafanyiwa kwa sababu walikuwa nje ya kituo cha mitihani tumewakamata saba na wengine 10 waliobakia jitihada za kuwatafuta zinaendelea ili wakamilike kulingana na idadi ya waliokuwa wanawafanyia mitihani,” alisema Kaimu Kamanda Dinya.

Alisema watuhumiwa hao 17 walighushi vitambulisho kuwawezesha kuingia kwenye chumba cha mtihani, akieleza vilikuwa na majina ya watahiniwa halisi.

“Mhadhiri mmoja alishtukia mfumo huo wa udanganyifu kufanyika ndipo walipoanza kufuatilia kwa sababu kuna picha za watahiniwa baada ya kuwachunguza hawa 17 walionekana si watahiniwa halisi, baada ya hapo walivijulisha vyombo vya dola na tukawakamata watuhumiwa hao,” alisema.

Kaimu Kamanda Dinya alisema baada ya kuwahoji watuhumiwa walidai waliingia makubalino na wanafunzi kuwafanyia mitihani kila ‘Paper’ kwa gharama ya kati ya Sh30,000 hadi Sh50,000.

Alipoulizwa iwapo watuhumiwa wamepewa dhamana, Kaimu Kamanda Dinya alisema:

“Kuhusu dhamana siwezi kulizungumzia sana japo dhamana ni haki ya mtuhumiwa lakini kwa kuwa kuna mkuu wa upelelezi na anaendelea na uchunguzi,  akikamilisha kazi yake, dhamana itakuwa wazi kwa kuwa ni haki yao.”

Alisema nafasi ya dhamana itakuwa wazi pale watakapojiridhisha kile wanachokitafuta kutoka kwa watuhumiwa hao kama vimepatikana kulingana na wanavyohitaji.

Profesa Bisanda juzi alisema chuo hicho kilianza mitihani Juni 3 hadi 24, na wanafunzi 10,417 walifanya mitihani katika vituo 53, ambavyo vimesambaa nchi nzima.

“Katika kipindi cha wiki tatu za mitihani, kwa umakini wa mifumo yetu, wasimamizi wa mitihani waliwakamata mamluki wapatao 17, hususani katika vituo vya Ilala na Kinondoni, Dar es Salaam. Matukio mengi yalibainika kuanzia Juni 18,” alisema Profesa huyo.

Alisema kitendo cha watu hao kughushi vitambulisho vya chuo na tiketi ya ukumbi wa mitihani ni vitendo vya jinai, hivyo sheria ichukue mkondo wake. 

Alisema waliokamatwa siyo wa chuo hicho, bali ni kutoka vyuo vingine na wengine ni wafanyakazi katika fani walizosomea.

Profesa Bisanda alisema chuo kina sheria na kanuni za mitihani ambazo zitatumika kuwashughulikia.

“Mamlaka za chuo zitawahoji wahusika na wakikutwa na hatia, basi wataadhibiwa kulingana na kanuni,” alisema.

Kwa waliofikishwa Polisi, alisema hataridhika kuambiwa wanaendelea na upelelezi, kwani maofisa wa Usalama wa Taifa walishuhudia matukio hayo hivyo hayahitaji upelelezi zaidi.

Ili kukomesha vitendo vya namna hiyo, Profesa Bisanda alisema OUT ipo kwenye maandalizi ya kuwasajili wanafunzi wote kwa alama za vidole, na kumhakiki kila mtahiniwa kwa mashine maalumu za utambuzi wa alama za vidole katika vituo vyote vya mitihani.

Akizungumzia hilo, mdau wa elimu, Dk Faraja Kristomus alisema changamoto iliyopo ni namna ya uendeshaji wa elimu masafa ambayo wanafunzi wenye nia ovu hutumia mwanya huo kufanya mambo yasiyofaa.

Alisema matokeo ya uhalifu huo ni nchi kuwa na watu wengi wenye vyeti vya kitaaluma lakini hawana maarifa, kwa sababu wana uwezo wa kuwalipa wengine wawafanyie kazi zao kitaaluma vyuoni.

“Haya mambo yanaonekana Chuo Kikuu Huria kwa sababu mfumo wake ni elimu masafa, watu wanasoma nyumbani wanaonekana wakati wa mitihani, jambo linalotoa mwanya kwa mamluki kujichomeka na wengi wanaopenda kupata njia za mkato wanakimbilia huko,” alisema.

“Athari zake ni kwamba, tutakuwa na watu wengi wasio na maarifa lakini wana vyeti vya kitaaluma na hii ni matokeo ya kuweka kipaumbele kwenye vyeti badala ya kupima maarifa ya mtu,” alisema.

Dk Kristomus alisema kitendo cha waajiri kuweka kipaumbele kwenye vyeti kinawafanya vijana wengi kuwekeza nguvu kwenye kupata vyeti na siyo maarifa ndiyo maana wengine wapo tayari kutoa pesa wafanyiwe mitihani na tafiti.

Alisema changamoto ipo pia serikalini ambako watumishi wa umma ili wapande vyeo, ni lazima wasome na kupata vyeti.

“Hii inawafanya watu wakimbilie Chuo Kikuu Huria kwa sababu wanajua watapata mwanya wa kuingiza watu wao wawalipe fedha wawafanyie mitihani na hata kuwaandikia tafiti. Tunazidi kutengeneza kizazi cha watu wasio waaminifu,” alisema Dk Kristomus.

Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet), Martha Makala, alisema kuna umuhimu mkubwa wa kudhibiti mfumo wa mitihani ili wanafunzi waweze kupimwa wao na kuwezesha Taifa kupata wasomi wenye ujuzi.

“Katika zama hizi ambazo tunazungumzia elimu ujuzi na ubunifu, lazima udhibiti uwe mkubwa ili kutengeneza watu watakaotusaidia kupiga hatua. Huwezi kuwa mbunifu kama unakwepa kipimo cha mtihani. Haya yakiendelea hatari yake ni kwamba tutapata wahitimu wasio na ujuzi,” alisema Martha.

Akizungumzia na Mwananchi juzi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Loisulie alisema kilichobainika ni sehemu ndogo ya matukio makubwa yaliyopo kwenye sekta ya elimu.

“Kilichotokea ni kidogo kati ya mengi yanayoendelea, watu wanaandikiwa tafiti na mazoezi kabla ya mitihani wanafanyiwa, hii inaonyesha mifumo ya usimamizi wa mitihani ni dhaifu sana,” alisema.

Dk Loisulie alisema matukio kama hayo ya watu kufanyiwa mitihani madhara yake yataonekana baadaye kwa watendaji wasio na uwezo kuingia kwenye soko la ajira.

Hoja hiyo iliungwa mkono na mdau wa elimu, Mustapha Puya aliyesema mifumo ya elimu ndiyo changamoto.

Alisema hilo siyo tukio la kwanza kwenye elimu akitoa mfano wa wanafunzi waliowahi kuhojiwa kwenye chombo cha habari na kukiri kufanyiana mitihani bila kubainika lakini hakuna hatua zilizotangazwa kuchukuliwa mpaka sasa dhidi yao

“Hao ni 17 tu kwenye vituo viwili wapo wengi ambao hawajakamatwa, hii maana yake ni kwamba tunaingiza wahitimu feki sokoni, ni muhimu OUT ikahakikisha inatumia mifumo ya kuwasajili wanafunzi kwa alama za vidole kumaliza changamoto hii,” alisema.

Related Posts