TETESI ZA USAJILI BONGO: Nahimana anajiandaa kusepa Namungo

KIPA wa kimataifa wa Burundi, Jonathan Nahimana anayeidakia Namungo huenda msimu ujao asiwe sehemu ya kikosi hicho baada ya kukichezea kwa miaka minne.

Inaelezwa Namungo haina mpango wa kumwongeza mkataba Nahimana ambaye aliichezea mechi 34 na mwenyewe ameanza kufikiria maisha mapya nje ya timu hiyo ya Kusini mwa Tanzania.

Namungo inatajwa kumalizana na kipa wa zamani wa Simba na Yanga Beno Kalolanya atakayetua kwa mkopo kutoka Singida Black Stars (zamani Ihefu) baada ya kumalizana na Singida Fountain Gate.

Bado Nahimana hajajua wapi atacheza msimu ujao na wakati huu dirisha liko wazi anaamini atapata timu na msimu ujao atacheza Ligi Kuu Bara.

Wakati huo huo Yanga Princess inadaiwa ipo mawindoni kumnasa kiungo mshambuliaji wa Simba Queens, Joelle Bukuru aliyemaliza mkataba na Wekundu hao. Mrundi huyo aliyeichezea kwa mkopo Fountain Gate Princess akitokea Simba alikuwa akipigiwa hesabu kuongezwa mkataba na Wekundu, lakini inaelezwa Yanga nao imeingilia kati ikimtaka pia kumnasa.

SIKU chache baada ya kutemwa na Simba, nyota wa kimataifa wa Burundi, Saido Ntibazonkiza inadaiwa yupo mbioni kurejea nchini kupigamoja ya timu za Ligi Kuu Bara. Awali ilielezwa Saido alikuwa akihitajika Rwanda, lakini upepo umebadilikla baada ya Coastal Union na Namungo zikitajwa sambamba na Pamba, Ken Gold na Dodoma Jiji zilizompeleka ofa akiwa mapumzikoni.

AZAM FC inadaiwa ipo mbioni kumpa nafasi nyingine winga Tepsie Evance baada ya kumaliza mkataba wake wa mkopo kwa KMC. Baadhi ya viongozi wa timu hiyo wanahitaji kumbakisha Tepsie aliyekulia kwenye akademi yao licha ya kuwa na shutuma za utovu wa nidhamu na sasa dili hilo linasubiri baraka za Kocha Youssouph Dabo kuamua.

JKT Queens imeanza mazungumzo na wachezaji wawili wa Fountain Gate Princess, kiungo Protasia Mbunda na beki Sara Joel. Wachezaji hawa wawili bado wana mkataba na klabu zao na huenda wakajiunga na wanajeshi hao kutokana na changamoto ya kifedha inayowaathiri Fountain.

SIMBA Queens na JKT Queens imeingia kwenye vita ya kumuwania kiungo wa Baobab Queens, Josephine Julius iliyoshuka daraja. Inavyoelezwa klabu zote mbili zimeweka ofa nzuri kilichobaki ni mchezaji mwenyewe kuchagua wapi atamwaga wino ilikukipiga msimu ujao kwenye Ligi Kuu ya Wanawake.

BAADA ya Mashujaa FC, kuachana na beki Juma Makapu imeelezwa anafanya mazungumzo na JKT Tanzania na Coastal Union ya Tanga, anaangalia ni wapi panaweza kuwa na maslahi naye. Inadaiwa kuwa mazungumzo yanayoendelea baina ya beki huyo na timu hizo na yoyote itakayomridhisha itambeba kwa msimu ujao.

KIPA wa Geita Gold iliyoshuka daraja, Constantine Malimi inadaiwa ana ofa mbili mkononi kutoka Kagera Sugar na Namungo FC, huku zikifanya mazungumzo ya awali ya kumnasa. Malimi aliyemaliza na clean sheet 10 na asisti moja msimu uliopita, anasikilizia tu kwa sasa timu itakayokubaliana naye kimasilahi ili aweze kusaini mkataba wa kuitumikia.

Related Posts

en English sw Swahili