WAKATI Simba ikiendelea kuweka mambo sawa katika dirisha hili la usajili linaloendelea, imeshusha chuma ambacho ujio wake unatajwa kuwa unakwenda kuleta changamoto kwa nahodha msaidizi wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ katika eneo analocheza la beki wa kushoto.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni baada ya miaka zaidi ya sita kupita ikimshuhudia Tshabalala akitamba atakavyo katika eneo hilo ambalo limekuwa pia likizalisha mabao kibao Msimbazi kutoka na krosi anazopiga beki huyo kutokea upande huo.
Lakini, msimu ujao utashuhudia beki mgeni wa kushoto, Valentino Nouma aliyekuwa anakipiga Saint Eloi Lupopo ya DR Congo akitua ili kusaidiana na nahodha huyo aliyeachiwa mikoba na John Bocco aliyesepa Msimbazi.
Nouma anaungana na Tshabalala ambaye alijiunga na Simba Juni 2014 akitokea Kagera Sugar ya Bukoba baada ya awali kuchezea pia akademi ya Azam FC.
Tshabalala ndiye mkongwe aliyebaki Simba ambaye anacheza nafasi hiyo na mara ya mwisho kuletewa mgeni ni kipindi ilipomsajili Asante Kwasi akitokea Lipuli ambaye alifanikiwa kutwaa taji akiwa na timu hiyo.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwanaspoti kuwa wamefanya uamuzi wa kumsajili mchezaji huyo akiwa huru baada ya kumaliza mkataba wake na timu yake kwa lengo la kuongeza nguvu eneo hilo.
“Tshabalala ni beki bora na amekuwa akifanya vizuri kwenye timu yetu na timu ya taifa. Tunatambua thamani yake kumuongezea nguvu ni kuhakikisha tunampa muda mzuri wa kupumzika ili aendeleze ubora,” kimesema chango hicho.
“Ujio wa beki huyo utaongeza ushindani na ubora eneo hilo hasa kipindi hiki ambacho klabu inatengeneza timu bora na ya ushindani, lakini pia itatoa mwanya kwa kocha kufanya mabadiliko kulingana na ubora wa mchezaji.”
Alipoulizwa juu ya mkataba waliompa beki huyo amesema wamemsainisha miaka miwili kutokana na umri alionao na wanaamini ni chaguo sahihi wakitarajia mambo makubwa kutoka kwake hasa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
“Kwa sasa unasomeka mwaka mmoja ambao utamfanya amalize wa pili kama ataonyesha kiwango bora ambacho tunakitarajia kutoka kwake, lakini hadi sasa kila kitu kimekamilika anaungana na timu muda wowote kabla ya timu haijasafiri kwenda Misri kwa kambi maalumu ya msimu mpya.”
Kwa sasa Tshabalala ana miaka 10 Msimbazi na amekuwa na ubora uleule licha ya kuletewa wachezaji mbalimbali wa ndani na nje waliochemka na kumuacha akiendelea.
Wachezaji walioletwa Simba wanaocheza nafasi ya beki wa kushoto ni wengi na wameshindwa kufurukuta na mmoja wao alikuwa ni Jamal Mwambeleko aliyesajiliwa na kikosi hicho akiwa na kiwango bora wakati akiitumikia Mbao FC.
Mwambeleko licha ya kiwango bora alichokuwa nacho akiwa na Mbao ya jijini Mwanza, lakini ujio wake Simba ulikuwa kama kaa la moto kwani alishindwa kupenya kwa Tshabalala na mwishoni aliomba kuondoka na kujiunga Singida United.
Mwingine ni Mghana Asante Kwasi alionekana huenda akapindua ufalme wa Tshabalala Simba wakati anasajiliwa 2017 akitokea Lipuli ya Iringa kutokana na ubora wake wa kuzuia na wakati huohuo kuanzisha mashambulizi hatari.
Kwasi alionekana ni mchezaji tishio ingawa alijikuta akishindwa kupigania namba na nyota huyo na baada ya kudumu misimu miwili aliondoka ndani ya kikosi hicho 2019 na kujiunga na Klabu ya Hafia ya Guinea.
Nyota mwingine aliyeingia kwenye mtego wa Tshabalala ni Gadiel Michael ambaye alijiunga na kikosi cha Simba 2019 akiwa ni chaguo namba moja akitokea Yanga ila mambo yalikuwa magumu kwake na baadaye kuondoka na kujiunga na Singida Fountain Gate, sasa anakipiga Cape Town Spurs FC ya Afrika Kusini.