Dar es Salaam. Matukio ya usafirishaji wa bidhaa kimagendo ikiwemo mafuta ya kupikia kutoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam kupitia pwani bahari ya Hindi yameendelea kushamiri.
Hilo limethibitishwa na Jeshi la Polisi Kikosi cha Wanamaji cha Dar es Salaam katika kipindi cha miezi sita kupitia operesheni zake mbili tofauti maalumu za kudhibiti uhalifu zilizofanywa katika ukanda huo.
Amesema jumla ya shehena 2731 za mafuta ya kupikia zenye ujazo wa lita 20 zimenaswa katika ukanda huo.
Shehena hizo zimekamatwa na majahazi matatu, pamoja na watuhumiwa nane waliokuwa wakijaribu kusafirisha bidhaa hizo wakiwa na lengo la kukwepa kulipa ushuru wa forodha.
Hii si mara ya kwanza kwa shehena ya aina hiyo kukamatwa, Januari 5, mwaka huu, jeshi hilo lilithibitisha kukamatwa kwa watu wanne wakiwa na shehena ya madumu 1,000 ya mafuta ya kupikia yenye ujazo wa lita 20 yakisafirishwa kutoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam na jahazi la Mv Huda.
Katika operesheni ya pili iliyofanyika kuanzia Mei hadi Juni, 2024 jeshi hilo limewatia mbaroni watu wanne akiwemo nahodha Masoud Rajabu kwa tuhuma za kubeba mafuta ya kupikia dumu 1731 zenye ujazo wa lita 20 kila moja wakiwa na nia ya kukwepa ushuru.
Watuhumiwa hao wamenaswa wakiwa kwenye majahazi mawili kwenye ukanda wa bahari ya Hindi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Juni 29, 2024 ya operesheni iliyofanyika kuanzia Mei hadi Juni, Kamanda wa Kikosi cha Polisi Wanamaji ACP, Moshi Sokoro amesema katika ufuatiliaji huo kikosi kazi cha polisi kilitumia boti na kufanikisha kuwakamata.
“Tumekamata majahazi mawili, Mv Ukimaindi Poa na jahazi lingine lisilokuwa na jina wala namba za usajili katika bahari ya Hindi, Dar es Salaam yakiwa na watuhumiwa wanne akiwemo nahodha Masoud Rajabu wakiwa wamebeba mafuta ya kupikia dumu 1731 zenye ujazo wa lita 20 kila moja wakiwa na nia ya kukwepa ushuru wa forodha.,”imesema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa maelezo ya kamanda Sokoro kupitia taarifa hiyo, uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini watuhumiwa hao hawakuwa na nyaraka zinazothibitisha uhalali wa umiliki wa mizigo hiyo ya mafuta ya kupikia pamoja na nyaraka za usafirishaji.
“Kikosi cha Polisi Wanamaji Dar es salaam tumefanikiwa kupeleka kesi saba mahakamani ambazo zipo katika hatua mbalimbali za kimahakama, na moja kati hizo mtuhumiwa amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka miwili au faini ya Sh2 milioni kwa makosa ya uvuvi haramu,”amesema
Kamanda Sokoro ametumia fursa hiyo kutoa onyo kwa wafanyabiashara wasio waadilifu kuacha kusafirisha mizigo kwa njia ya bahari bila kuwa na nyaraka za mizigo hiyo.