Wanafunzi wa ukaguzi kunolewa nchi nzima

Dar es Salaam. Wadau wa masuala ya ukaguzi wa ndani, wameanza safari ya kuwajengea uwezo na ujuzi wanafunzi wa vyuo vikuu nchini wanaosomea fani hiyo ili kuwapata wakaguzi bora, wenye weledi na maadili kwa ajili ya siku za usoni.

Hayo yameelezwa Juni 28, 2024 na mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakaguzi wa Ndani ya Dunia, Emmanuel Johannes katika mkutano wa kwanza wa jumuiya ya wanafunzi wanaosomea fani ya ukaguzi wa ndani wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, (UDSM).

mkutano huo uliokuwa na kauli mbiu ya “Kuwezesha vizazi vijavyo vya wakaguzi wa ndani” uliwakutanisha wadau sekta hiyo.

Miongoni mwa mambo waliojadiliana ni namna wanafunzi hao wanavyoweza kujiandaa kwa mustakabali wa baadaye wa fani ya ukaguzi wa ndani, maadili na ujuzi.

“Tumewaambia mambo  kuhusu ukaguzi na changamoto zilizopo, matumizi ya teknolojia, wao kama wanafunzi wanajiandaaje. Pia, tumewaambia wanatakiwa kuongeza ujuzi ili kukabiliana na changamoto za ajira siku za mbele,” amesema Johannes.

Johannes amesema sehemu kubwa ya changamoto zilizopo katika ukaguzi wa ndani ni kukubalika, akisema hakuna mtu anayetaka kukaguliwa mara kwa mara na kwamba sio watu wote wanaokubaliana na taarifa ya ukaguzi.

Johannes amesema wameanzia UDSM lakini mpango mkakati wao, ni kuongeza wigo wa kufika katika vyuo vikuu vingine nchini.

Hata hivyo, Johannes amesema mpango huo una gharama, kwa hiyo wanatafuta vyanzo vya mapato vya kuwezesha mchakato huo.

“Huko nyuma kulikuwa na mjadala watu wanapaswa kufundishwa maadili, maana muda mwingine watu wanasema kuna upigaji wa hapa na pale. Sasa wakati huu ndio tunawaandaa vijana wetu kuwa waadilifu watakaowajibika katika Taifa.

“Katika hivi vyuo, ndiyo sehemu sahihi, tunachokifanya haya ndiyo maandalizi, matarajio yetu kuwafikia wanafunzi wengi kadri tuwezavyo. Kwa kufanya hivi tunaandaa wakaguzi wa ndani watakaoitumikia nchi kwa uadilifu zaidi,” amesema Johannes.

Rais wa Wakaguzi wa Ndani, Zelia Njeza amesema wamechukua jitihada hizo ili kuwaandaa wanafunzi kuwa bora.

“Jitihada kama hizi zimekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo mwamko wa wanafunzi kujiunga jumuiya za wakaguzi wa ndani za vyuo vikuu. Tumekuwa na maombi mbalimbali ya vyuo vikuu vikiomba kuanzishwa jumuiya kama hizi katika vyuo vyao.

“Tupo tayari kuwaunga mkono vijana ili kupata wakaguzi wazuri baadaye, tunawaanda katika mambo mengi, kujifunza kuhusu ukaguzi wa ndani, uongozi na kuzingatia misingi yetu,” amesema Njeza.

Njeza amesema kazi ya ukaguzi wa ndani sio rahisi kama watu wanavyodhani, lazima mtu awe na utaalamu wa hali ya juu kuhusu fani hiyo.

“Tunataka kuwaandaa vijana ili wakiingia mtaani wasiyumbe katika kutafuta kazi, lakini katika mchakato huu tunaita wadau mbalimbali tunaoshirikiana kwa lengo la kuwashika mkono wanafunzi hawa hasa kupata mafunzo kwa vitendo,” amesema.

Mwanzilishi wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Daines Mbao,  amesema pamoja na mambo mengine wanahamasisha wanafunzi kusomea fani hiyo ili kuwa wakaguzi wa ndani kwa siku za usoni.

“Katika mkutano huu wa siku mbili tunawapa elimu na ujuzi ili kuwa wakaguzi bora wa ndani wa baadaye,” amesema Mbao.

Related Posts