Wanawake watafuta kadi zaidi ya moja kwa ajili ya mtoto na kuwapa wanaume ili wasaidie malezi

Ili kuimarisha makuzi na malezi ya watoto na kutengeneza kizazi salama,wanawake wametakiwa kuacha kuwatumia watoto kama biashara kwa kutengeneza kadi zaidi ya moja na kuwakabidhi wanaume ili waweze kusaidia kwenye malezi ya mtoto kwa kudhani ni wa kwake.

 

Wito huo umetolewa na Felisia Hyera mratibu wa mama na mtoto mkoa wa Njombe kwenye kikao cha utekelezaji wa programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto (PJT-MMMAM) unaotekelezwa na shirika lisilo la kiserikali la UWODO kwa kushirikiana na serikali ambapo awali Godfrey Kiowi ambaye ni afisa maendeleo ya jamii halmashauri ya wilaya ya Njombe alieleza namna wanavyokutana na kesi ya mtoto mmoja kuwa nana baba wanne huku akiomba serikali kuona namna ya kubadili mfumo wa upatikanaji wa kadi za watoto.

“Hizi kesi tunakutana nazo huko mtaani mtoto mmoja ana baba wanne lakini pia ukija kufuatilia kila baba amepewa kadi yake na kila baba anatoa huduma kwa muda wake halafu kesho linaibuka kila baba anasema mtoto ni wa kwake”amesema Kiowi

Felisia ametoa wito wanawake kuwa waaminifu ili kutengeneza familia bora kwa kuwa wengi wanaofanya hivyo hutokana na kushindwa kukubaliana na uhalisia wa mimba walizobeba hali inayopelekea mtoto kuanza kuyumbishwa tangu akiwa tumboni kwa mama.

 

“Siku zote huwa tunasisitiza mjamzito afike kliniki akiwa na ujauzito wa chini ya miezi mitatu na hausemi lazima uende kituo x sasa mama huyu akifika ambapo mimi nipo nitamfungulia kadi lakini hatujui mama huyu wakati wa makuzi yake ilikuweje anaamua kwenda kituo kingine tena kule nako watampa kadi nyingine na kama bado hajatimiza akina baba aliokuwa nao atajitahidi kwenda kwenye vituo kulingana na idadi ya wababa alio nao”amesema Felisia

Kwa upande wake Hamis Kassapa ambaye ni mkurugenzi wa shirika la UWODO amesema katika kikao walichokaa na wataalamu mbalimbali wameweza kuwajengea uwezo juu ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ili kwenda kuendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali za watoto kwenye makuzi amabapo pia amehimiza wazazi na walezi kutenga muda wa kukaa na watoto na kuwajenga kwenye ulinzi pamoja na afya ili waweze kuwa na afya wakati wa makuzi yao.

Related Posts