Dar es Salaam. Wakati wananchi wa Mtaa Mpya, Kata ya Ulongoni B, wakileza kuwa na wasiwasi wa bomba la gesi asilia lililopita maeneo hayo kuwa wazi kufuatia kuzolewa kwa mchanga juu yake, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), limesema bada bomba hilo ni salama
Bomba hilo ndilo linalosafirisha gesi asilia kutoka Mtwara kupeleka katika kituo kikuu cha kuipokea na kuisambaza gesi hiyo kilichopo Kinyerezi jijini humo.
Akizungumza jana Ijumaa Juni 28,2024, Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni tanzu ya TPDC, inayoshughulika na uendeshaji na ukarabati wa miundombinu ya gesi (Gasco), Baltazar Mrosso, amekiri kuwepo kwa hali hiyo, huku akiwataka wananchi kutokuwa na wasiwasi kwani bado lipo salama kwa namna lilivyo.
“Ni kweli bomba letu lilipata madhara ya mchanga uliokuwa umelifunika mita mbili kwenda chini kusombwa na maji kipindi cha mvua za El-Nino, na sasa hivi ukipita eneo hilo unaliona.
“Ila halina shida kwa kuwa madhara yanayoweza kutokea endapo lipo hivyo au limefunikwa ni sawasawa kutokana na mgandamizo wa presha isiyopungua bar 70 unaosafirisha gesi hiyo asili, hivyo kama ingekuwa hatarishi madhara yake yangeshaonekana, lakini ukweli ni kwamba lipo salama,”amesema Mrosso.
Hata hivyo, amesema hali ya mchanga juu ya mabomba hayo kuzolewa, haijatokea tu Ulongoni, pia yapo maeneo mengine korofi ambapo linapita ikiwemo mto Tegeta na Goba, lakini hata huko mikoa ya Mtwara na Lindi gesi inapotokea..
Akieleza hatua walizochukua hadi sasa, Mrosso, amesema wapo katika mpango wa kulikarabati kwa kulijengea kuta ambazo hata maji ya mvua yakipita mengi halitaathirika na walichokuwa wanasubiri ni maji ardhini yapungue baada ya mvua zilizomalizika hivi karibuni.
Vilevile maeneo ambayo yamechubuka rangi ambayo ni maalumu kwa ajili ya kulilinda lisipate kutu, wanaendelea kuparudishia pamoja na kuongeza vifusi kwa kuvifunga na kamba ngumu ili maji yanapokuwa mengi lisisukumwe.
Wakizungumza na Mwananchi, wananchi wamesema tangu bomba hilo liwe wazi, wanapata wasiwasi kuhusu usalama wao na hasa pale wanapolisikia wakati mwingine likitoa harufu ya gesi.
Fatuma Musa, amesema awali wakati bomba hilo limewekwa lilikuwa chini ya ardhi limefunikwa halionekani, lakini kadri mvua zinaponyesha limekuwa likipanda juu na uchafu ikiwemo magogo yanapopita eneo hilo huwa linasukumwa na hivyo kuwa na hofu.
Mosi Abdallah, amesema wasiwasi wao mkubwa ni kutokana na njia huyo kuitumia kwenda hospitali, huku akiomba Serikali kuangalia namna ya kulifanya.
“Hii sio mara ya kwanza kwa bomba hilo kubomoka, kwani ilishawahi kutokea hivyo wakaja kuweka zege, likaondoka na mvua, mara ya pili hivyihivyo. Sasa hivi wakijenga itakuwa mara ya tatu, usalama wetu hapa uko wapi, Serikali itusaidie kwa kuwa yenyewe ndio mtetezi wetu,”amsema Mosi.
Ally Hassan, amesema kama bomba hilo ni zima kwa nini kuna maeneo limewekwa viraka kwa kufungwa vitambaa, na pia limevimba tofauti na ilivyokuwa awali hivyo kuomba kuchukuliwa hatua kabla halijaleta madhara kwa watu.
Kuhusu viraka, Mrosso amesema sio kweli bali ni kamba ambazo zinashikilia vifusi vilivyochimbiwa chini kulishikilia bomba lisiyumbe maji yakipita.
Akizungumzia hilo, Mjumbe wa serikali ya Mtaa, Fatuma Mpeta, amesema malalamiko hayo wananchi yalimfikia naye kuyawasilisha ngazi za juu ambapo wananchi waliandika barua kwenda kwa mkuu wa Wilaya ya Ilala.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, alipoulizwa kuhusu hilo alikiri kupokea barua ya wananchi hao na kueleza alizungumza na wenye bomba na kumhakikishai halina madhara.
“TPDC walishasema hilo bomba halina madhara, nadhani kinachopaswa kufanya ni kuendelea kutolewa kwa elimu kwa wananchi hao, ili pia waweze kulilinda ili wenye nia ovu wasije wakatumia kama fursa kulihujumu,”amesema Mpogolo.