Iringa. Miili ya watu wanne wakiwemo watoto watatu waliofariki kwenye ajali ya bodaboda, imezikwa katika makaburi ya Karielo mjini Iringa huku waombolezaji wakigubikwa na huzuni wakati wa maziko hayo.
Kwa mujibu wa maelezo wa ndugu wa marehemu, Ramadhani Said amesema watoto wawili na dereva bodaboda ni familia moja na mtoto mwingine ni wa jirani.
Msiba huo uligubikwa na simanzi kwa ndugu, jamaa na marafiki waliojitokeza kuwahifadhi wapendwa wao ambapo wamesema hilo limekuwa pigo kubwa kwa wanafamilia na jamii kwa ujumla kwa kuondokewa na wapendwa wao kwa wakati mmoja.
Watoto hao na dereva wa bodaboda, walifariki dunia papo hapo mjini Iringa Juni 28, 2024 baada bodaboda iliyowabeba watoto hao kugongwa na lori la mizigo aina ya Faw, mali ya kampuni ya TransAfrica.
Akizungumza baada ya kuwahifadhi wapendwa wao, msemaji wa familia, Ramadhani Said amesema watoto hao ni wajukuu zake na alipata taarifa akiwa shambani akarudi na kukuta watoto hao wamefariki.
“Mkubwa aliyekuwa anaendesha pikipiki ni mjomba wao na hawa wawili wadogo walitoka Ipogolo kwenda Mjini kwa mama yao na kila Ijumaa ilikuwa ni lazima waende kwa mama yao.
“Huyu mtoto mwingine ni wa jirani yetu na wamekuwa pamoja kila wakati, huyu mtoto wa jirani alichukukiwa ili awashikilie wale watoto wadogo wakiwa kwenye pikipiki,” amesema Said.
Awali, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Alfred Mbena alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo akisema ilitokea usiku wa juzi, Juni 28, 2024 saa 1 usiku katika eneo la Mlima Ipogoro, kata ya Kitanzini, kwenye Barabara Kuu ya Iringa – Dodoma.
Kamanda Mbena amesema pikipiki ambayo ilisabisha ajali hiyo, iliyokuwa ikiendeshwa na Hassan Burhan (17), ilitoroshwa muda mfupi mara baada ya ajali hiyo kutokea.
Alisema abiria waliokuwa wamebebwa katika pikipiki hiyo ni Helena Thomas (12), Ally Tenywa (9) na Gabriel Gongo (5), wote wakiwa ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Ipogoro.
Alisema pikipiki hiyo iligonga ubavuni upande wa kushoto wa gari lenye namba za usajili RAG450N/RL 5167.
Alisema lori hilo lilikuwa ikitokea Ruvuma kuelekea Dodoma, likiendeshwa na Said Rashid (27), mkazi wa Dar es Salaam na kusabisha vifo kwa watu wanne akiwemo dereva pikipiki na abiria wake watatu.
Kamanda huyo ameongeza kuwa kutokana uchunguzi uliofanyika, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa pikipiki kujaribu kulipita lori hilo upande wa kushoto na kuligonga ubavuni na kuanguka na kisha kukanyagwa na magurudumu ya nyuma.
Amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo, wamesema imetokea baada ya bodaboda huyo kujaribu kupita kwenye upande usio wake na baada kupoteza mwelekeo ndipo lori hilo lilipowagonga.