Zanzibar ilivyopokea watalii 400 moja kwa moja kutoka Hispania

Unguja. Zanzibar imepokea watalii 400 kutoka nchini Spain ikiwa ni safari ya kwanza ya moja kwa moja.

Hatua hiyo inatajwa kuongeza idadi ya watalii kisiwani humo.Wamesafiri kwa Shirika la Ndege la World to Fly

Hayo yamesemwa leo Juni 29, 2024 na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Khalid Salum Mohamed alipowapokea watalii hao katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume.

Waziri Khalid amesema huo ni uthibitisho kwamba Zanzibar inazidi kufahamika duniani na hayo ndiyo matunda ya kujitangaza.

“Kwa sasa tuna mashirika 80 ambayo yanaleta ndege zake kisiwani hapa na shirika hili ndiyo mara ya kwanza kuleta watalii moja kwa moja hapa, huu ni wigo mpana katika soko la utalii,” amesema.

Amesema ujio wa ndege hiyo utachangia kuongeza pato la Taifa na kuleta ustawi kwa wananchi.

Waziri wa Utalii Zanzibar, Ramadhani Mudrik Soraga amesema hilo ni soko jipya, hivyo watahakikisha wanatanua wigo wa utalii.

Soraga amesema kupitia soko hilo jipya wanatarajia wageni wasiopungua 10,000 watakaofika Zanzibar kwa shughuli za utalii.

Amesema wanaendelea kujipanga kwa kuboresha huduma na kuwawekea mazingira mazuri kwa vile wanavyovihitaji.

Soraga amesema changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni idadi ndogo ya watalii wanaotembelea Zanzibar lakini hawarejei, hivyo wanataka kuhakikisha hilo linaondoka.

“Tuna mkakati wa kuhuisha maeneo ya kale na kuyafanya kuwa ya utalii wa kiutamaduni. Tunapaswa kuyatumia maeneo hayo,” amesema Soraga.

Khamis Ali Suleiman, kutoka Kampuni ya Safari Tour amesema ujio wa ndege hiyo utaongeza fursa za utalii na kwa wananchi kwa ujumla.

Related Posts