Zawadi Mauya afunguka yaliyojificha Yanga

KIUNGO aliyemaliza mkataba Yanga, Zawadi Mauya ameizungumzia misimu minne ndani ya kikosi hicho jinsi ilivyompa upana wa kufanya kazi yake kwa weledi, licha ya kushindwa kuanika dili la kutua Singida Black Stars (zamani Ihefu) inayodaiwa kumpa mkataba wa miaka miwili.

Mauya alijiunga na Yanga, Julai Mosi 2020 ambapo msimu ulioisha alimaliza mkataba na Mwanaspoti limepata taarifa za kusaini mkataba wa miaka miwili na Singida Black Stars, japo mwenyewe amechomoa kuzungumzia kwa sasa kwa madai kwamba jambo hilo lipo chini ya menejimenti inayomsimamia.

Alisema kwa muda aliokaa Yanga alikuwa na wakati mzuri wa kujifunza mambo mengi yatakayomsaidia kwenye taaluma yake popote atakapokuwa.

“Yanga ni klabu iliyo na mipango mikubwa. Kama mchezaji nilijifunza kuendana nayo, nimepata ujuzi kwa makocha tofauti, kitendo cha kucheza wazawa na wageni kimeniongezea mambo mengi katika majukumu yangu. Kikubwa naamini ninachokifanya siyo wanachokiona wengine kwangu,” alisema.

“Zipo alama nyingi za kumbukumbu nzuri kutoka katika klabu ya Yanga siwezi kutaja moja baada ya nyingine, ingawa kwa msimu ulioisha sikuwa na nafasi kubwa ya kucheza, hivyo haukuwa mzuri kwangu uwanjani, ila ulikuwa bora kwa klabu kunyakua mataji yote muhimu.”

Alisema ndoto zake za kuvaa medali za ubingwa zimetimia akibeba na timu hiyo misimu mitatu mfululizo ndoo ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho na Ngao ya Jamii mbali na Kombe la Mapinduzi 2022, hivyo kilichobaki ni kuendelea kupambana kuonyesha ubora wake katika timu ambayo ataichezea msimu ujao.

Mauya alijiunga na Yanga akitokea Kagera Sugar iliyomsajili pia kutoka Lipuli ya Iringa na tangu atue Jangwani alikuwa mmoja ya wachezaji waliokuwa wakitumika kufukia mashimo pale timu inapokuwa na mchezo mgumu katika eneo la katikati.

Pia aliwahi kuitungua Simba katika mechi ya Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Julai 03, 2021 baada ya awali kuahirishwa kitatanishi Mei 8, mwaka huo na yeye kufunga bao dakika ya 12.

Related Posts