Abuni kifaa cha kuongeza usikivu cha bei nafuu

Dar es Salaam. Huenda watu wenye changamoto ya usikivu wakapata ahueni zaidi, baada ya mwalimu wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) kubuni kifaa kinachoweza kuwasaidia kusikia vizuri.

Kubuniwa kwa kifaa hicho nchini, kutashusha gharama za ununuzi ambazo watu wenye changamoto hiyo walikuwa wakizipata katika kununua vifaa kutoka Sh 500,000 kwa kifaa cha sikio moja cha analogia na Sh1.2 milioni kwa kifaa cha kidigitali.

Innocent Maziku, mbunifu wa kifaa hicho amesema changamoto ya usikivu aliyokuwa akipambana nayo ndiyo ilimsukuma kutafuta suluhisho lake. Amezungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili, Juni 30, 2024 katika Maonyesho ya 48 ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF).

Amesema alipata changamoto hiyo ghafla alipokuwa darasa la sita, ilimfanya kupata tabu katika masomo yake huku kifaa alichonunuliwa hospitalini wakati huo kikishindwa kumsaidia.

“Kwanza kilikuwa gharama, pamoja na kununuliwa kilishindwa kunisaidia kwa sababu nilikuwa nikipita sokoni au sehemu yenye watu wengi siwezi kumudu kelele zake, niliachana na kifaa hicho nilipomaliza darasa la saba,” amesema Maziku.

Hali hiyo ilimlazimu kutumia usikivu kidogo alionao katika ngazi zote za masomo hadi alipomaliza chuo kikuu na kuajiriwa Veta Kigoma mwaka 2018.

“Nilipoajiriwa nilianza kuangalia namna ambayo naweza kupata suluhu ya suala hili, nilianza kufanya ubunifu taratibu na miaka miwili nyuma nilianza kufanikiwa, Machi mwaka huu ndiyo nikafikia hapa,” amesema Maziku.

Amesema kifaa hicho kinachouzwa Sh100,000 kimetengenezwa katika namna ambayo mtu huweza kuongeza au kupunguza sauti yeye mwenyewe kulingana na namna anavyohitaji.

“Namna nilivyotengeneza ni sawa na vile vinavyouzwa hospitali, tofauti yake ni ukubwa pekee, ila kila kitu kilichomo katika vifaa vinavyotolewa hospitalini,” amesema Maziku.

Yeye ni mnufaika namba moja wa kifaa hicho huku akiendelea kuangalia namna anayoweza kupata wataalamu wa kukifanyia vipimo kuangakia uimara wake na jinsi kinavyoweza kusaidia jamii.

“Lengo langu ni kusaidia kundi kubwa la watu ambalo halina uwezo wa kumudu gharama za vifaa vya usikivu vinavyotolewa hospitali mbalimbali nchini,” amesema Maziku.

Hata hivyo, ameleza kuwa kifaa hicho huweza kumsaidia mtu ambaye usikuvu wake ni hafifu pekee, si walio na matatizo mengine ya masikio kama wale wanaoweza kusikia sauti, lakini wanashindwa kuelewa kinachozungumzwa.

Kutokana na hilo, Mwananchi ilifika katika banda la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na kukuta vifaa maalumu vya kuongeza usikivu vikiuzwa kwa kati ya Sh500,000 kwa vile vya analogia hadi Sh1.2 milioni kwa vile vya kidigitali.

Akizungumzia ubunifu uliofanyika, mtaalamu wa usikivu, kizunguzungu, msawazo, matamshi, lugha na kuongea kutoka MNH, Fikiri Idd amesema ubunifu huo ni mzuri kwa awali, kwani umefanyika nchini.

Hata hivyo, amemtaka Maziku kupeleka kifaa chake Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), ili kipimwe kujua ubora wake.

“Hata yeye tunamshauri asikitumie sana, apeleke kipimwe, ili kujua asilimia za ubora wake kwa ajili ya matumizi na atashauriwa nini cha kupunguza au kuongeza, ili kupata kilichokuwa bora,” amesema Idd.

Kufanya hivyo kutasaidia kupata bidhaa bora itakayoendana na mahitaji ya wagonjwa kwa kile alichokisema kuwa mtu akiwa na matatizo ya usikivu huwa kuna viwango ambavyo huzingatiwa.

Related Posts