Alliance, Harab Motors tishio Ligi ya Caravans

LIGI ya Kriketi ya Caravans T20 ilikuwa njema kwa timu za Alliance Caravans na Harab Motors baada ya timu hizo kupata matokeo mazuri katika michezo iliyochezwa kwenye viwanja vya Dar Gymkhana na Anadil Burhan jijini Dar es Salaam mwishoni mwa juma.

Mechi ya kusisimua sana ya mwishoni mwa juma iliwakutanisha Alliance Caravans na Generics Gymkhana katika mchezo ambao Akhil Anil wa Alliance alikuwa nyota baada kuifungia timu yake jumla ya mikimbio 42 kati ya 127 iliyoiwezesha Alliance kushinda kwa jumla mikimbio 32.

Alliance ndio walioshinda kura ya kuanza, waliamua kuanza kwa kufunga, na waliweza kutengeneza mikimbio 127 huku wakipoteza wiketi saba.

Jitihada za timu ya Generics Gymkhana kuzifukuzia alama hizo hazikufua dafu baada ya wote kutolewa wakiwa na mikimbio 95 huku wakipoteza wiketi nane.

Moto mkali pia uliwaka katika mduara wa Anadil Burhan ambao ulishuhudiwa vijana wa Harab Motors wakiwasambaratisha wenzao wa Econo Lodge kwa ushindi wa wiketi 4 katika mchezo wa mizunguko 20 Jumamosi jioni.

Econo Lodge ndiyo walioshinda kura ya kuanza na wao kuamua kufunga, na azimio hilo liliwapelekea wao kutengeneza mikimbio 91 huku wakiangusha wiketi tisa.

Wakitumia mizunguko 9 tu, Vijana wa Harab Motors waliweza kuzifikia na kuzizidi alama hizo baada ya kufunga mikimbio 93 huku wakiangusha wiketi 6.

Mapema Ijumaa, kulikuwa pia mechi kabambe ya vijana kwenye uwanja huo.

Waliong’ara walikiwa ni Serengeti Boys walioibuka kidedea dhidi ya Kilimanjaro Boys kwa mikimbio 55 katika mchezo wa mizunguko 10 ambao ilikuwa ni maalum kwa ajili ya kutengeneza timu ya Taifa ya Kriketi kwa Vijana wasiozidi umri wa miaka 19.

Serengeti Boys walioshinda kura ya kushambulia, walitengeneza mikimbio 145 huku wakiangusha wiketi 10, alama hizo, hata hivyo zilionekana kubwa kwa vijana wa Kilimanjaro Boys ambao walimudu kutengeneza mikimbio 90 tu baada ya wote kutolewa.

Mashindano haya yanalenga kukuza kriketi nchini.

Related Posts