Dar es Salaam. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameiagiza Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) kuwasimamisha vigogo wawili wa mamlaka hiyo, akiwamo Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu, Kiula Kingu kupisha uchunguzi dhidi yao.
Mbali na Kingu, mwingine ni Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Maji wa Dawasa, Shaban Mkwanywe. Waziri Aweso ametoa maagizo hayo leo Jumapili, Juni 30, 2024, makao makuu ya Dawasa, Ubungo jijini Dar es Salaam, katika kikao cha pamoja kilichoketiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, wajumbe wa bodi na mameneja wa taasisi hiyo.
Awali Aweso alifanya ziara katika maeneo ya Chuo Kikuu cha Ardhi, Mbezi, Mshikamano na Tegeta A ambako kuna matenki ya maji.
Waziri Aweso amesema katika kipindi hicho cha mpito taasisi hiyo itakuwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Maji.
Sababu za kuwekwe kando ni utendaji usioridhisha ikiwemo kukosekana kwa maji kwenye matanki ya kuhifadhia na kusababisha malalamiko kwa wananchi ilihali maji kwenye vyanzo yapo na huduma ya umeme inapatikana muda wote.
“Mtendaji Mkuu changamoto hii ya uzalishaji wa maji unaifahamu na nilishakupa maagizo ya kuchukua hatua tena nilikutajia majina lakini hujachukua matokeo yake mnafanya kazi kirafiki ‘kishikaji’. “Nilikuagiza ukaonane na Katibu Mkuu kwa zaidi ya mara tatu hukuwahi kufanya hivyo na Katibu Mkuu alifanya ziara hapa viongozi hamkuonekana, kirahisi tu,” amesema.
Katika maelezo yake Waziri Aweso amefananisha kitendo cha kutokupatikana huduma hiyo na kila kitu kipo ni hujuma kwa taasisi hiyo na kutaka kuiharibia Serikali kwa wananchi wake wanaolalamikia maji.
“Lazima nichukue hatua Bodi nawaomba msimamisheni Mhandisi Shaban na tutafuatilia kwa nini uzalishaji anaosema hauakisi kwenye matenki ya kuhifadhia maji. Kama maji mtoni yapo na umeme upo kwa nini maji kwenye matenki hakuna na watu hawapati maji.”
“Bodi naomba pia msimamisheni Mtendaji mkuu kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake nilimuagiza lakini yupo kimya anafanya kazi kindugu wanashindwa kutambua tunawalipa mshahara kwa kodi za Watanzania,” amesema.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Jenerali mstaafu Davis Mamunyange amesema katika ziara tuliyofanya maeneo machache tuliyotembelea imetupa picha sahihi ya hali halisi ya huduma ya maji.
“Hali ya utoaji huduma ya maji kwa kweli ni mbaya na ziara ilikuwa ya kushtukiza na aliyofanya Katibu Mkuu ilikuwa ya kushtukiza zinafaa zaidi kuliko zile rasmi kwa kuwa watendaji wanakuwa wamejiandaa.
“Mimi sikutarajia na wajumbe wenzangu wa bodi tutakuta hali hiyo imetustua. Ni jambo ambalo hatukulitarajia na hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa,” amesema.
Jenerali Mamunyange amesema kama bodi watakaa kikao na kufanyia kazi maagizo yaliyotolewa na waziri huyo kwa kuzingatia utaratibu wa bodi hiyo.
Akizungumza katika mkutano huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma amesema uwajibikaji wa watendaji kwenye taasisi hiyo hauridhishi huku akieleza maji yanayopotea ni mengi.
“Maji yanapotea mengi, hakuna kiongozi anayechua hatua, katika ziara niliyofanya siku mbili nimebaini mengi kwanza mifumo ya maji imeharibika lakini hakuna matengenezo pia hata flow mitter hazifanyi kazi kabisa,” amesema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko amesema licha ya maeneo mengi ya wilaya yake kufikiwa na miundombinu ya maji lakini malalamiko ni mengi.
“Niombe watendaji fanyeni kazi kwa kutafsiri na maono ya Serikali kwa vitendo, malalamiko ya wananchi ni mengi ni vigumu kuwaelewesha na wakakuelewa,” amesema.