Moscow. Rapa wa Kimarekani asiyeishiwa vituko kila kukicha, Kanye West ameripotiwa kuwepo jijini Moscow nchini Russia.
Kuwapo kwa nyota huyo wa muziki kutoka nchini Marekani, kumeripotiwa na vyombo vya habari vya nchini humo leo Jumapili, Juni 30, 2024 vikimnukuu mtayarishaji maarufu wa muziki wa nchini humo, Yana Rudkovskaya.
Kanye yupo nchini humo wakati wasanii wengi wa Magharibi hawajatumbuiza katika nchi hiyo baada ya mashambulizi yake Ukraine ambayo yalisababisha vikwazo vya Marekani na Ulaya dhidi ya Russia, pamoja na vizuizi vya kusafiri kwenda nchi hiyo.
Kanye West, ambaye amezua utata kwa kauli zake za kisiasa nchini Marekani na hivi karibuni alishutumiwa kwa kumsifu Adolf Hitler, ameeleza kufurahiwa na Rais Vladimir Putin.
“Kanye West tayari yuko Moscow. Hizi ni habari njema, anakaa katikati mwa mji mkuu,” shirika la habari la TASS limemnukuu mtayarishaji Yana Rudkovskaya aliyeeleza kwenye mtandao wa kijamii.
Aidha, Shirika la Habari la AFP limesema, tangazo la mtayarishaji Rudkovskaya lilifuatia baada ya uvumi wa mwezi uliopita kwamba Kanye West atafanya tamasha Moscow.
Lakini taarifa zilizopo ni kuwa uongozi wa uwanja wa Luzhniki wa Moscow ambao kulikuwa na uvumi wa rapa huyo angetumbuiza, hauna habari juu ya tamasha linaloweza kufanywa na rapa huyo maarufu.
Kanye West amekuwa mtu wa kugonga vichwa vya habari na mkewe Bianca Censori kutokana na mitindo yao ya mavazi ambayo mara nyingi inaishangaza ulimwengu.