TIMU ya kikapu ya wanaume ya Kigoma na wanawake ya Mara zimeibuka mabingwa wa mashindano ya Kikapu ya Taifa (CRDB Taifa Cup) yaliyomalizika juzi Jumamosi usiku kwenye Uwanja wa Chinangali, jijini Dodoma.
Kigoma ilishinda taji hilo kwa kuifunga Dodoma kwa pointi 58-54, ilihali Mara ilipata ushindani mkali kuifunga Unguja kwa pointi 57-56 katika mchezo wa kusisimua.
Kigoma na Mara kila moja zilizawadiwa kitita cha Sh7 milioni kutoka kwa wadhamini wa mashindano hayo, Benki ya CRDB na kikombe.
Dodoma iliyoingia mara ya pili mfululizo katika fainali hiyo kwa upande wa wanaume, ilizawadiwa Sh4 milioni, huku Unguja kwa wanawake ilizawadiwa pia kiasi kama hicho cha Sh4 milioni.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule aliwazawadia washindi zawadi hizo kwa kushirikiana na rais wa Shirikisho la mpira wa kikapu la Tanzania (TBF) Michael Kadebe na Emmanuel Kiondo ambaye ni Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa benki ya CRDB.
Kwa upande wa wanawake, Nelious Mbugeni wa Arusha alishinda tuzo ya ‘Best Rookie wa mwaka na kwa upande wa wanaume, Minja Riad Msuya wa Mtwara alishinda tuzo hiyo na kila mmoja alizawadiwa Sh200,000.