Dar es Salaam. Aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa amejiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) na kutambulishwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC).
Mchungaji Msigwa aliyewahi kuwa mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, ametambulishwa leo Jumapili Juni 30, 2024 katika kikao hicho kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, kikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan.
Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi ndiye aliyemshika mkono Mchungaji Msigwa na kuingia naye katika ukumbi uliokuwapo wajumbe wa NEC, walionekana wakishangiliwa baada ya kada huyo na mwanasiasa machachali kuingia ukumbi humo.
Baada ya kutinga ukumbini hapo zilianza kusikika nyimbo zikisema mlete Msigwa…huku mwanasiasa huyo akionekana kutabasamu na kupiga makofi.
Mei 29, 2024 Mchungaji Msigwa ambaye ni mbunge wa zamani wa Iringa Mjini alishindwa kutetea uenyekiti wa kanda ya Nyasa, baada ya kubwagwa na Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu kwa tofauti ya kura mbili.
Hata hivyo, baada ya kushindwa uchaguzi huo, Mchungaji Msigwa aliyewahi kuwa kada wa NCCR-Mageuzi alisema ataendelea kukitumikia Chadema, akisema hakuingia chama hicho kwa ajili ya uongozi na aliahidi kumpa ushirikiano Sugu.
Maoni katika mitandao ya kijamii
Fuatilia zaidi katika mitandao yetu……