Morogoro. Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Juma Nzigula, mkazi wa Peapea, Kata ya Ludewa, Wilaya ya Kilosa mkoani hapa, amefariki dunia baada ya kudaiwa kupigwa rungu kisogoni na mfugaji wa jamii ya Kimasai.
Inadaiwa kuwa Mmasai huyo alimpiga Nzigula baada ya kudai kummulika kwa tochi usiku wakati akitoka kwenye majukumu yake.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Juni 30, 2024, mke wa marehemu, Esta Juma amesema alipata taarifa za kifo cha mumewe baada ya kupigiwa simu na mtoto mkubwa wa kaka wa marehemu.
“Kifo hiki kilitokea tarehe 28 Saa 12 jioni, nilikuwa ndani na mtoto wangu, nilipigiwa simu, nilipopokea nikasikia sauti ya mtu mwingine akisema mume wangu amepigwa fimbo na Mmasai haongei. Nilianza kupiga kelele na watu walikuja kunisaidia na kuniuliza kuna nini,” amesimulia Esta kwa uchungu huku akibubujikwa na machozi.
Amesema siku hiyo mumewe alienda kutafuta kuni za kupikia nyumbani kwa sababu yeye amejifungua siku 14 zilizopita.
“Kwa hiyo mume wangu akasema ngoja akatafute kuni za kupikia hapa nyumbani wakati anarudi ndiyo haya yamemkuta,” amesema Esta.
Akizungumzia mauaji hayo, Juma Chadali, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Peapea Kilabuni, amesema kifo cha Nzigula kinadaiwa kusababishwa na ugomvi uliotokea baada ya Mmasai kudai amemulikwa kwa tochi usoni kwa muda mrefu.
Amesema Nzigula alipigwa rungu kisogoni na alifariki dunia kabla ya kufikishwa Hospitali ya Wilaya ya Kilosa alikokuwa anapelekwa.
“Kwa sasa, ndugu wa marehemu kutoka Kahama, Shinyanga wanakuja Kilosa kuungana na wengine kwa ajili ya kupanga utaratibu wa kusafirisha mwili kwa maziko huko Shinyanga,” amesema Chadali.
Naye jirani wa marehemu, Mussa Kumwenda ameiomba Serikali kumkamata na kumchukulia hatua kali aliyefanya tukio hilo, akisisitiza kuwa matukio kama hayo yanahatarisha usalama katika kitongoji chao.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amesema Serikali imeanza kumtafuta aliyesababisha mauaji hayo na vyombo vya ulinzi viko kazini kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa.
Shaka amewahakikishia wananchi kuwa hawatavumilia matendo maovu kama hayo yaendelee kutokea wilayani humo na kuwataka wasitumie tukio hilo kutia doa wilaya yao.