Dar es Salaam. Baada ya ukimya wa siku sita tangu alipoadhibiwa kutohudhuria vikao 15 vya Bunge, Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina ametangaza mpango wa kuwaburuza mahakamani Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.
Pamoja na Dk Tulia, mbunge huyo amesema hatua kama hizo atazichukua dhidi ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) na kampuni zote zilizopewa jukumu la kuagiza sukari.
Mbunge huyo aliadhibiwa na Bunge Juni 24, 2024 kutohudhuria vikao 15 vya Bunge hadi Novemba 2024, kwa kosa la kuidharau mamlaka ya Spika na Bunge kwa ujumla.
Uamuzi wa kuadhibiwa kwake umetokana na Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Ally Makoa kulielea Bunge kwamba, Mpina amekutwa na hatia ya kudharau mamlaka ya Spika na mwenendo wa shughuli za Bunge.
Mzizi wa yote hayo ni tuhuma zilizoibuliwa naye dhidi ya Bashe kuhusu uagizaji wa sukari, jambo lililosababisha Dk Tulia amtake awasilishe ushahidi.
Kilichomtia hatiani ni hatua yake ya kuwasilisha ushahidi wa tuhuma hizo kwa Dk Tulia, kisha kwenda kuziweka wazi katika mkutano wake na waandishi wa habari alioufanya muda mchache baada ya kukabidhi ushahidi huo kwa Spika.
Kutokana na adhabu hiyo, Mbunge huyo aliyewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, amesema ameonewa na hakupewa nafasi ya kusikilizwa ipasavyo na hata kamati imemuadhibu bila kujielekeza katika sheria na kanuni.
“Nimeamua kupeleka malalamiko yangu ya kuonewa na kutotendewa haki na Spika Tulia kwenye vyombo vya sheria, pia kumpeleka mahakamani Waziri wa Kilimo Hussein Bashe na Bodi ya Sukari chini ya ibara ya 26 na 27 kwa kutoa idhini ya kuagiza sukari kinyume cha sheria,” amesema katika mkutano wake na wanahabari.
Kuhusu madai ya Mpina kutotendewa haki na kusudi la kwenda mahakamani, Spika wa Bunge Tulia alipotafutwa kwa nyakati tofauti leo Jumapili Juni 30,2024, kwa simu ya mkononi iliita bila kupokelewa.
Alipotafutwa Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi azungumzie uamuzi huo wa Mpina, ameomba atumiwe ujumbe mfupi wa maandishi na hata alipotumiwa hakujibu. Alipopigiwa tena simu yake iliita bila majibu.
Mbali na hao, Mwananchi limemtafuta Waziri Bashe hakupatiana. Vivyo hivyo kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Makoa naye hakupatikana. Msingi wa kutafutwa kwao ni kuguswa na Mpina kwenye maelezo yake.
Akizungumzia hatua ya Mpinga kwenda mahakamani Mwanasheria, Clay Mwaifani amesema ni kugonganisha mihimili.
“Huo ni mtego kupeleka masuala ya Bunge mahakamani, kwa sababu Bunge lina sheria zake labda kinachoweza kufanyika ni kuangalia hukumu kama ilikuwa ya haki, lakini masuala ya Bunge si ya kisheria ni ya kisiasa hivyo kesi yake ni ngumu,”amesema.
Mwanasheria huyo amesema kama spika katika rekodi zake wabunge anaowapeleka kwenye kamati ya maadili wanakutwa na hatia hilo linaibua wasiwasi juu ya utendaji wa kamati husika.
Amesema ukosoaji alichofanya Mpina ndio wabunge wanapaswa kufanya lengo kuisimamia Serikali lakini kwa sasa upepo umebadilika wengi wao wanaisifia Serikali.
Jana Jumamosi, Juni 29, 2024, Mpina akizungumza na waandishi wa habari alisema taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ya Juni 24, 2024 kuhusu mbunge huyo kumdharau spika na Bunge ilikuwa na kasoro.
Amesema kamati kupitia taarifa yake ilieleza kurejea nakala halisi za taarifa ya spika na kujiridhisha vifungu vya 26 (d) na (e) na 34 (1) na (g) cha sheria haki na madaraka ya Bunge na kanuni ya 81 (j) na (k) ambavyo vinaeleza makosa aliyotuhumiwa kufanya.
Hiyo ni tofauti na vifungu vya 29(d) na (e) na kifungu cha 34 (1) na (g) cha sheria ya kinga, haki na madaraka ya Bunge sura 296, ambayo Spika Tulia alivitaja mbunge huyo kuwa kosa lake ni kinyume na vifungu hivyo.
Mpina amesema zipo tuhuma zilizoongezwa kutoka kifungu cha 26 (d) na (e) na kanuni 84 1 ya (j) (k) akihoji ni wapi vifungu hivyo vimetolewa wakati hazikuwepo kwenye tuhuma za spika.
“Kifungu cha 29 (d) na (e) cha sheria ya haki, kinga na madaraka ya Bunge ambayo spika alirejea kunituhumu nazo, hakiendani na maudhui ya tuhuma iliyotolewa na spika bali kifungu hicho kinaelezea makosa ya waandishi wa habari kuingia kwenye vikao vya Bunge bila kufuata utaratibu,” alieleza.
Kwa hoja hiyo, Mpina alisisitiza kifungu hicho hakitengenezi jinai dhidi yake na si sahihi Spika Tulia kumtuhumu kwa makosa ya waandishi wa habari wakati yeye ni mbunge.
Jambo lingine alilosema Mpina, hakuna kifungu cha 29 (d) katika sheria ya kinga, haki na madaraka ya Bunge sura 296 hivyo kunaibua maswali kwa nini Spika amtuhumu na kumuhukumu kwa kifungu cha sheria ambacho hakipo na makosa ya nidhamu ambayo hayapo.
Eneo la adhabu, Mpina alidokeza taarifa ya spika ilielekeza apewe adhabu chini ya kifungu cha 83(2) ambapo (a) alitaka mbunge huyo aonywe na kujirekebisha, (b) mbunge huyo kutoka nje ya kikao kwa muda uliobakia na (c) kumsimamisha vikao visivyozidi 10 mfululizo.
“Bila kujali kuwa kanuni hiyo inataja adhabu tatu tofauti, spika kutumia kipengele cha tatu na kuacha vipengele vya awali, hii inaacha tafsiri spika ilielekeza kamati aina ya adhabu itakayotolewa, hatua ambayo inainyima kamati uhuru wa kumshauri aina ya adhabu kulingana na aina ya kosa lenyewe,” alisema.
Dosari nyingine aliyoibua Mpina, ni namna wasilisho lake dhidi ya Bashe limehusishwa kumvunjia heshima Spika Tulia.
Amebainisha wasilisho lake halikuhusiana na mwenendo wa Bunge wala kamati yake bali tuhuma za uongo ndani ya Bunge.
Mbunge huyo wa Jimbo la Kisesa alisema, kuzungumza kwake na waandishi wa habari hakuna ukiukwaji wowote wa sheria alioutendana hata sheria iliyotumika kumuadhibu haipo.
“Kanuni ya 84(1) (j) inahusika na matendo yanayohusisha hadhi ya Bunge na sio mtu au mamlaka yeyote, maelezo niliyoyatoa hakuna namna yeyote yapoligusa Bunge wala kuishushia hadhi mamlaka yeyote,” alisema.
Akigusia dosari kwenye taarifa ya kamati, Mpina alisema haikuambatanisha utetezi wake alioutoa jambo linalothibitisha kamati hiyo ilizingatia hukumu ya spika bila kupewa nafasi ya kusikilizwa na kuhukumiwa kwa vifungu ambavyo havipo.
Suala la Spika kupendekeza adhabu iwe kufungiwa vikao 10, Mpina ametafsiri ndio kauli iliyotumiwa na kamati kumpa adhabu akisisitiza kamati yenyewe haikuwa huru.
“Alichokifanya wakati akitoa taarifa yake, alitoa adhabu na hukumu siku hiyo hiyo, ndipo akasema mkamsikilize, sasa nikasikilizwe nini wakati kaishasema nitafungiwa vikao 10,” alisema.
Mpina alieleza kuwa Spika kuwa ndio alikuwa mlalamikaji jambo linaloibua maswali.
Kuhusu kuvuja baadhi ya nyaraka kabla ya kufika bungeni, Mpina alisema nyaraka zile ni zake na spika hakueleza sababu za kuvuja kabla ya muda wake, akihoji kwa nini taarifa za mbunge zisizo rasmi zichukuliwe kwa jazba.
“Nyaraka za Serikali huwa zinavuja, nyaraka za Bunge zinavuja na hakuwahi kuja na jazba kiasi hicho, kilichompa jazba kwa taarifa zangu ambayo sio za siri ni nini na kunihukumu kabla ya kunisikiliza,” alihoji Mpina.
Kutokana na kutokuwa na kanuni ya kuonyesha makosa yake Mpina alisisitiza kuwa hajatenda kosa lolote.
Mpina alisema kasoro zilizojitokeza wakati wa mjadala wa azimio la Bunge Juni 24, ni taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kutokuwa sehemu ya shughuli za Bunge.
Jambo hilo, Mpina alibainisha liliwafanya wabunge kutokuwa na taarifa ya kile kilichowasilishwa.
“Kwenye ‘Order Paper’ hakuna mahala spika alisema kamati ya haki, kinga na madaraka ya Bunge itawasilisha bungeni taarifa, ghafla tuliambiwa inawasilishwa wabunge hawakujiandaa kwa sababu haikuwa kwenye ‘Order Paper’, utaratibu wetu, shughuli zinazotakiwa kwenda kuanza bungeni taarifa inatoka siku moja kabla au asubuhi ili wabunge wajiandae,” alisema.
Jambo la pili, Mpina alisema Spika Tulia hakutoa mwongozo wa namna ya uchangiaji wa taarifa ya kamati ya haki kinga na madaraka ya Bunge badala yake alisema ana majina ya wabunge watakaochangia bila kutoa utaratibu wa uliotumika kuwapata wachangiaji na taarifa haikuwa inafahamika bungeni.