Msigwa arusha kombora Chadema, wamjibu lilikuwa ni suala la muda tu

Dar es Salaam. Mbunge wa zamani wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa amesema uamuzi wake wa kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM) umechochewa na hatua ya Chadema kukosa misingi na uhalali wa kukikosoa chama hicho tawala.

Katika mazingira hayo, amesema hakuona haja ya kuendelea kushindana, badala yake aungane na Serikali katika mambo inayoyafanya ikiwamo amani, utulivu na uhuru wa kuzungumza.

Msigwa ametoa kauli hiyo leo, Jumapili Juni 30, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutangazwa kuwa mwanachama mpya wa CCM.

“Kwa kuwa tumepoteza misingi na tumekosa uhalali wa kuikosoa CCM, watu wenye akili, nimeona ni bora niungane na CCM,” amesema.

Amesema Chadema inapoteza agenda ya kuwavutia wananchi, akieleza kimebaki kudandia vitu.

Katika maelezo yake hayo, amesema atashirikiana na makada wengine wa CCM kuzunguka nchi nzima kueleza juu ya usanii na uongo wa Chadema kwa wananchi.

“Tunaongea kuhusu demokrasia ndani ya chama hakuna demokrasia, tunaongea kuhusu ufisadi ndani ya chama kuna ufisadi, tunaongea kuhusu haki ndani ya chama hakuna haki,” amesema.

Kilichomshinda ndani ya Chadema amesema ni kuendelea kuvumilia kuwadanganya wananchi kwamba CCM ni mbaya ilhali viongozi ndani ya chama hicho cha upinzani ndiyo wabaya.

Hata hivyo, amesema uamuzi wake wa awali wa kujiunga na Chadema ulitokana na kuvutiwa na misingi ambayo kwa sasa haipo tena.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema katika maelezo ya chama hicho juu ya Msigwa kutimkia CCM amesema intelejensia ya Chadema ilishatoa taarifa ya mwenendo wake na kulikuwa na dalili zote za Msigwa kujiunga na chama tawala.

“Tulikuwa tunasubiri muda ufike na muda umefika leo, kwa sababu ameamua kwenda CCM, tunaendelea kukijenga chama chetu,” amesema.

Mrema alizihusisha harakati za Msigwa katika siku za mwishomwisho ndani ya Chadema na vurugu za maandalizi ya kupandisha thamani yake ili aondoke.

Katika msisitizo wa kauli yake hiyo, amesema: “Hata uko CCM Mchungaji Msigwa akikosa cheo ataondoka.”

Kuhusu rufaa yake ya kupinga ushindi dhidi ya Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu aliyemshinda kwenye uchaguzi wa uenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Mrema amesema ilikuwa isikilizwe katika kikao cha Baraza Kuu, kwa sababu mwanasiasa huyo alikuwa mjumbe wa kamati kuu.

“Tulikuwa tunasubiri chaguzi zote zimalizike ndipo tuitishe baraza kuu kujadili rufaa ya Msigwa, tusingeweza kujadili rufaa yake pekee maana huenda zingine zingejitokeza na kufanya vikao mara kwa mara vya baraza kuu ni gharama,” amesema Mrema.

Kwa uamuzi huo wa Msigwa, amesema mchakato wa kusikiliza rufaa yake utakuwa umejifia hapo.

Uamuzi wa Msigwa, umemuumiza Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema aliyesema angetamani kubaki kuwa naye ndani ya chama hicho.

“Nilitamani tuendelee naye kufanya kazi, lakini ni uamuzi wa mtu huwezi kuuzuia, Msigwa alikuwa ni kama kaka yangu, nilitamani tuendelee kuwa timu moja (Chadema),” amesema Lema ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema kama alivyokuwa Msigwa zamani.

Related Posts