Mwanafunzi Veta abuni mashine ya makuzi ya watoto njiti

Dar es Salaam. Katika kusaidia makuzi ya watoto njiti na kukabili changamoto zao, mwanafunzi wa Chuo cha Mafunzo na Ufundi Stadi (Veta), George Nyahende, amebuni mashine ya kuwakuzia watoto hao yenye mzani, mpira wa gesi na taa za kusaidia kupambana na magonjwa ya ngozi.

Mashine hiyo itaondoa usumbufu wa watoto kutolewa kila wanapokutana na changamoto za upumuaji na magonjwa ya ngozi kwa kupelekwa katika mashine nyingine zilizohifadhiwa sehemu maalumu.

Akikzungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Juni 30, 2024 katika Maonyesho ya 48 ya Kimataifa ya Dar es Salaam, Nyahende amesema mashine hiyo itasaidia usalama kwa mtoto njiti kutokutolewa mara kwa mara na kuachwa katika ukuaji ulio salama na kufanyiwa matibabu husika akiwa ndani ya mashine hiyo.

“Kwa utafiti niliofanya hospitali, mfano za Arusha ambazo zinatumia mashine za kukuzia watoto zilizotoka nje ya nchi asilimia kubwa watoto wanatolewa wanapokuwa na changamoto ya upumuaji na magonjwa ya ngozi na wanatembezwa kwa haraka kufikishwa kwenye eneo husika. Hii si salama kwa mujibu wa wataalamu wa tiba,” amesema Nyahende.

Pia, amesema mashine inayotengenezwa katika kiwanda cha ndani ni rahisi kwenye matengenezo kwa kuwa muhusika anakuwepo, tofauti na zile za nje zinatakiwa kurudishwa zilipotoka na Serikali kutumia gharama nyingine za usafirishaji.

Ili kutofautisha mashine hiyo na nyingine, aliangalia changamoto zinazowakabili watoto njiti kwenye ukuaji na kugundua kwenye upumuaji kunahitajika uwekezaji na kuweka kifaa kitakachosaidia upumuaji na magonjwa ya ngozi.

Amesema katika kuhakikisha mashine hiyo ipo kwenye ubora, ameshirikiana na Taasisi ya Afya Ifakara na amepitia katika ofisi zote za Serikali ambazo zinahusika na masuala ya usajili na kutoa vibali, ikiwepo Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) na kupatiwa cheti cha umiliki wa mashine hiyo kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO).

Aidha, amesema gharama ya mashine aliyotengeneza haitazidi Sh10 milioni, tofauti na za nje ambazo gharama zake ni zaidi ya Sh80 milioni.

Kwa upande wake, daktari bingwa wa magonjwa ya watoto njiti, Dk Lucy Mpayo amesema kutengenezwa kwa kifaa kinachotumika kutibu tatizo zaidi ya moja itarahisisha matibabu kwa watoto wenye uhitaji.

“Watoto njiti wana mahitaji mbalimbali na vifaa vinavyotumika ni zaidi ya kimoja, ni gharama hivyo kama Watanzania wamebuni kitu kitakachowasaidia watoto hao itakuwa ni nafuu,” amesema Dk Lucy.

Kwa mujibu wa Dk Lucy, kwa mwaka wanazaliwa watoto njiti 200,000 na wanakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Pia, amesema ili kupunguza changamoto za vifaa tiba kwa watoto, ni muhimu kuwaunga mkono wabunifu wanafanyakazi za ubunifu za kusaidia matibabu.

Aprili 7, 2024 wataalamu sita wa fani ya uhandisi wa vifaa tiba “Biomedical Engineering” nchini, waliungana na kubuni mashine ya kuhifadhi watoto waliozaliwa kabla ya wakati ‘Phototherapy Machine’ yenye uwezo wa kutoa tiba nne tofauti kwa mtoto hao.

Mashine hiyo yenye uwezo wa kutoa joto kama la tumboni mwa mama, kutibu ugonjwa wa manjano, kuonyesha joto na uzito wa mtoto, imebuniwa na wahandisi hao kupitia kampuni mpya ya Tiba Labs wakishirikiana na madaktari bingwa wa watoto wachanga na madaktari bingwa wa wanawake na uzazi.

Related Posts