Dar es Salaam. Nyumba 100 zilizojengwa awamu ya kwanza na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika mradi wa Samia Housing Scheme maeneo ya Kawe, Dar es Salaam zimeshanunuliwa zote kabla hazijaisha, huku ikiliingizia shirika hilo Sh31 bilioni.
Hayo yamesema leo Jumapili Juni 30,2024 na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Hamad Abdallah alipokuwa akitoa taarifa kwa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, iliyofanya ziara ya kutembelea miradi mitatu mikubwa inayotekeleza na shirika hilo jijini humo.
Miradi walioitembelea wabunge hao ni wa Samia uliopo, Seven Eleven (711) yote ikiwa Kawe na ule wa Moroco Square ukiopo Kinondoni.
Akizungumzia mradi wa Samia Housing Scheme, Abdallah amesema nyumba zake zimeshanunuliwa. “Kutokana na kununuliwa mapema tumeokoa riba ya asilimia 13 ambayo tungepaswa kuilipa kama tungekopa fedha zote za ujenzi, badala yake tulikopa Sh5 bilioni pekee.”
“Mradi huu ni utekelezaji wa kujenga nyumba 5,000 ya watu wa vipato vya kawaida, unagharimu Sh466 utakuwa na nyumba 560 na hizo 100 zilizoanza kujengwa ni kwa ajili ya awamu ya kwanza na ndio tayari zote zimeshanunuliwa wakati zikiwa katika hatua mbalimbali ya ujenzi,” amesema Abdallah.
Mkurugenzi huyo amesema nyumba hizo ambazo ni kati ya nyumba 5,000 zitakazojengwa ndani ya uongozi wa Rais Samia Hassan Suluhu, kwa ajili watu wa kipato cha kawaida bei yake zinaanzia Sh38 kwa chumba kimoja cha kulala, Sh192 milioni kwa vyumba viwili vya kulala na Sh160 milioni yenye vyumba vitatu vya kulala.
Nyumba hizo zinatarajiwa kujengwa katika mikoa mbalimbali nchini ambapo asilimia 30 zitajengwa jijini Dodoma na asilimia 20 iliyobaki zitajengwa mikoa mingine nchini.
Kuhusu mradi wa Seven eleven, Abdallah amesema umesimama kwa miaka minane iliyopita lakini Rais Samia baada ya kuingia madarakani Machi 19, 2021 aliridhia kuchukuliwa mkopo wa kuuendeleza na wakati umesimama ulikuwa umefika ghorofa saba ila kwa sasa ghorofa zilizopo ni 12.
Kwa upande wa mradi wa Moroco Square, amesema nyumba 71 kati ya 100 za makazi zimeshauzwa huku maeneo kwa ajili ya maduka makubwa (shoping mall) washapangisha kwa asilimia 78 na tayari sehemu ya hoteli yenye hadhi ya nyota tano yenye vyumba 81, mmiliki wake King Jada ameshaanza kutoa huduma tangu miezi miwili iliyopita.
Akizungumzia ziara ya kamati ya Bunge, Mkurugenzi huyo amesema kwao ni faraja kwa kuwa wameenda kushuhudia fedha wanazoziomba namna gani wanazifanyia miradi yenye tija kwa Taifa.
Akifanya majumuisho ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge, Timotheo Msava amesema wamefurahishwa na kuridhishwa na namna miradi inavyotekelezwa.
“Kwa kweli niseme tumefurahishwa sana na kuridhishwa na miradi hii, ukizingatia ni kati ya miradi ambayo mmoja unaenda kuacha alama ya Rais Samia kwenye nchi hii.
“Lakini miradi miwili ya Seven Eleven na Moroco ni katika kuhakikisha shirika linatafuta fedga kwa ajili ya kujiendesha na kamati tunaamini kazi hizi zisingefanyika vizuri kama sio maono ya Rais Samia kukubali kutoa fedha kuikamilisha,” amesema Mzava.
Hata hivyo, ametoa wito kwa NHC kuwa asingependa kuona miradi inasimama tena kwa kisingizio cha kutokuwa na fedha kilishamalizwa na kutaka ikamilike kwa wakati uliopangwa.
“Miradi inaposimama inaiongezea gharama Serikali, hivyo ikamilike kama ilivyopangwa.”
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda ameahidi wizara kuendelea kusimamia miradi hiyo ili imalizike kwa wakati na kuleta tija.
Pia amewakaribisha Watanzania kununua sehemu hizo za makazi na sio kusubiri hadi jengo likamilike jambo litakalowaepusha kuuziwa kwa bei ya juu na waliowatangulia.