Sarah awasha moto Msoga Marathoni

WAKATI Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete akiwaita wanariadha kujifua mjini Msoga na kuahidi kuwapa sapoti, mwanariadha maarufu nchini, Sarah Ramadhan ameibuka mshindi wa mbio za Msoga Marathoni zilizofanyika wikiendi iliyopita, huku akifuatiwa na mkali mwingine Failuna Abdi.

Tuanze na JK. Rais Kikwete aliyeongoza mbio ya Msoga Half Marathoni iliyofanyika kwa mara ya kwanza mjini humo wilayani Chalinze, mkoa wa Pwani.

Mbio hizo zilianzia njiapanda ya Msoga na kumalizikia kwenye viwanja vya Shule ya Mmsingi Msoga zikilenga kukusanya fedha za kusaidia afya ya mama na mtoto kwenye hospitali ya wilaya ya Chalinze.

Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi kwa washindi, Rais Mstaafu Kikwete alisema yuko tayari kuwasapoti wanariadha watakaokwenda kujifua Msoga, huku akizungumzia mbio hizo, alikiri zimekuwa na mwanzo mzuri.

“Sikutegemea watu wengi namna hii washiriki, imekuwa na mwanzo mzuri,” alisema JK.

Katika mbio hizo, nyota wa timu ya taifa ya riadha, Sarah Ramadhan aliibuka kinara kwa wanawake akitumia saa 1:10:29:48 kumaliza kilomita 21, akifuatiwa na Failuna Abdi, aliyetumia saa 1:12:12:18 wote wa Arusha na Angelina John wa Singida alihitimisha tatu bora akitumia saa 1:12:28:73.

Kwa upande wa wanaume, Joseph Panga wa JWTZ alikuwa kinara wa mbio hizo za Km21 akitumia saa 1:02:06:86, Dickson Paulo wa Mwanza alimaliza wa pili akitumia saa 1:02:55:28 na Josephat Gisemwa wa Arusha aliyetumia saa 1:03:30:21 alimaliza wa tatu.

Kwa upande mbio za kilomita 10 kwa wanawake, Elizabeth Ilanda alikuwa kinara akitumia dakika 37:59:64 akifuatiwa na Sarah Hitii aliyetumia dakika 38:07:86 wote wa Arusha na Warda Shaban wa Singida alimaliza watatu akitumia dakika 39:25:04.

Kwa wanaume, Jumanne Mnada wa Arusha aliyetumia dakika 31:25:30 alikuwa kinara akifuatiwa na Inyasi Sulle aliyekimbia kwa dakika 31:41:58 na Marco Silvester aliyetumia dakika 31:53:16 alihitumisha tatu bora, wote wa JWTZ.

Rais Kikwete alikabidhi zawadi ya pesa taslimu pia kwa mshindi wa nne hadi wa 15 wa nusu marathoni (kilomita 21) na mshindi wa nne hadi wa 10 wa kilomita 10 kwa wanaume na wanawake. Pia alikabidhi zawadi kwa wazee wa zaidi ya miaka 50 waliomaliza tatu bora za kilomita 10.

Related Posts