Dar es Salaam. Hatimaye Edgar Mwakabela, maarufu Sativa anayedaiwa kutoweka Juni 23, 2024 na kupatikana mkoani Katavi, amewasili jijini Dar es Salaam na amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa matibabu zaidi.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Juni 30,2024 mmoja wa watu wa karibu waliompokea mgonjwa huyo, Boniface Jacob amesema wanamshukuru Mungu Sativa amefika salama jijini Dar es Salaam.
“Ameshaanza matibabu yupo Aga Khan ingawa alikuwa analalamika maumivu makali sana hasa sehemu alizojeruhiwa na watu waliomteka na kumtesa,” amesema Jacob ambaye ni meya wa zamani wa Manispaa za Kinondoni na Ubungo.
Sativa mkazi wa Mbezi wilayani Ubungo alipatikana Alhamisi Juni 27, 2024 katika pori la Hifadhi ya Taifa ya Katavi akiwa na majeraha mwili, akiomba msaada wa kupelekwa hospitalini.
Baada ya kupatikana katika pori hilo, Sativa alipelekwa Kituo cha Afya Mpimbwe kisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi.
Hata hivyo, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyanyi alisema jeshi hilo linafanya uchunguzi tukio la Sativa kupigwa kisha kutupwa kwenye msitu huo.
“Hivi sasa anaendelea na matibabu wakati uchunguzi wa tukio hili ukiendelea kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kiuchunguzi,” alisema Kamanda Ngonyanyi.
Juni 27, 2024 baada ya kuokotwa katika pori la Katavi, Sativa alionekana akivuja damu huku akilalamika maumivu makali ya kichwa na sehemu za mwili wake baada ya kupigwa na watu waliomteka.
Pia, Sativa anayejishughulisha na biashara ya miamala ya fedha, alilalamika kuvimba miguu huku taya ya upande wa kulia likivunjwa, akiwaomba wasamaria wema hao kumpeleka hospitali.